Habari

Mwanamume auawa kwa risasi kwenye farakano lililomhusisha Aisha Jumwa

October 16th, 2019 1 min read

Na CHARLES LWANGA

MWANAMUME aliuawa Jumanne kwa kupigwa risasi nyumbani kwa mgombea wa ODM wa kiti cha udiwani Wadi ya Ganda Ruben Katana kwenye patashika inayomhusisha mbunge wa Malindi Aisha Jumwa.

Hii ni baada ya fujo kutokea baina ya wafuasi wa Jumwa na wa chama cha ODM eneo la Ganda, Kaunti ya Malindi.

Mkasa huo ulitokea Penduliani, nyumbani kwa Ruben Katana.

Tayari Jumwa na watu wengine wanne wamekamatwa.

Bw Katana na viongozi wengine inadaiwa walikuwa wakikutana na maajenti kwa matayarisho ya uchaguzi mdogo wa Alhamisi.

Aliyepigwa risasi ni mjombake mgombea huyo wa ODM.

Duru zinasema Jumwa na wafuasi wake waliingia kwa boma hilo kukiwa na madai kwamba viongozi wa ODM walikuwa wanakutana na vijana wa eneo hilo.

Mapema, maafisa wa polisi walikuwa wameingia katika boma hilo. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikuwa imeratibu Jumatatu kwamba ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kampeni.

Hata hivyo, maafisa walitoa usalama baada ya kutaarifiwa kwamba mkutano haukuhusiana kivyovyote vile na kampeni.

Saa moja baadaye, Jumwa na wenzake waliwahi pahala hapo na kulazimu maafisa kulipua vitoa machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wanasababisha rabsha.

Mwanamume mmoja aliyeshuhudia ameambia wanahabari kwamba fujo zilitokea Jumwa na walinzi wake walipofika hapo.

“Jumwa alionekana mwenye ghadhabu na aliingia licha ya maafisa kumzuia kuingia palipoandaliwa kikao cha faragha,” alisema mwanamume huyo.

Jumapili, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna pamoja na Naibu Gavana wa Mombasa William Kingi na mwenzake wa Kilifi Gideon Saburi walimpigia debe mgombea wa ODM.

Jumwa anamuunga mkono mgombea wa kujitegemea Abdul Omar.

Kiti kiliachwa wazi baada ya kufutwa kwa matokeo yaliyomwidhinisha Abdulrahman Omar.