Mwanaume ajitia kitanzi kwa wakwe zake Homa Bay
MWANAUME mwenye umri 32 kutoka kijiji cha Magare, Kaunti ya Homa Bay wikendi alijitia kitanzi nyumbani kwa babamkwe baada ya kukosana na mkewe.
Eric Omondi aliondoka Nairobi ambako anaendesha biashara kisha kusafiri hadi Lokesheni ya Kanyabala, Homa Bay Magharibi ambako alikatiza uhai kwenye boma la babamkwe.
Mwili wake uligunduliwa na shemeji yake wakati ambapo familia ilikuwa ikijiandaa kumkaribisha. Babamkwe Pater Aluoch alisema mwanaume huyo alifika nyumbani mwake bila kutarajiwa.
Walikuwa ndio wameamka walipofahamishwa na jirani kuwa Omondi alikuwa akitafuta nyumba ya wakwe zake na alikuwa amewauliza wanakijiji mbalimbali mahali boma hilo lipo.
“Huwa tunazungumza tu kwa simu na amekuwa akiishi na mwanangu kama mkewe kwa muda wa miaka minane iliyopita. Kwa kuwa alikuwa mgeni tuliamua kumkaribisha na mke wangu alikuwa akiandaa chai ili tunywe pamoja,” akasema Bw Aluoch.
Omondi aliomba ruhusu kidogo aonge na jamaa zake ambao walikuwa njiani, akajificha na kujitia kitanzi kwenye mti bomani humo. Familia waliosikitishwa na kisa hicho waliwaarifu polisi ambao walikuja kisha wakauchukua mwili.
Polisi waligundua alikuwa na kamba tatu na alitumia moja kujitia kitanzi. Bw Aluoch alithibitisha kuwa mwanawe alikuwa amemwaarifu walikuwa wakigombana na mumewe.
Wanakijiji walisema mauti hayo ni nuksi kwao na huenda wakapatwa na janga iwapo tambiko halitafanyika. Walisema mwanaume huyo angekumbatia mazungumzo na wakwe zake kupata suluhu kwa ugomvi kati yake na mkewe badala ya kujitia kitanzi bomani humo.
“Hatujazoea matukio kama hayo na mara nyingi tumeyasikia yakifanyika maeneo mengine,” akasema Dan Odhiambo.
Naibu Chifu wa Kanyabala Kaskazini Washington Kidew aliungana na polisi kuchukua mwili huo ambao ulihamishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.