Habari

Mwanaume pabaya baada ya uume wake kudungiwa kemikali Meru

Na DAVID MUCHUI July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAUME mmoja kutoka Tigania ya Kati, Kaunti ya Meru analilia haki baada ya kudungwa kwenye sehemu nyeti kwa kemikali kwa tuhuma za kuiba miraa.

Shadrack Muriira kutoka kijiji cha Kilindo, Tigania ya Kati alinyakwa kisha muuguzi kutoka Hospitali ya Mikinduri akamdunga kwa kemikali hiyo kwenye korodani.

Muuguzi huyo alidai alimdunga kwa kemikali hiyo ili kumaliza ‘kizazi chake cha wezi sugu’.

Akiwa na umri wa miaka 18 pekee, Bw Muriira anakumbuka kuwa mnamo Juni 27 alikuwa akielekea katika kituo cha kibiashara cha Kilindoni karibu na nyumba yake alipovamiwa na wanaume watatu ambao walimuingiza kwenye gari kwa lazima.

“Waliniambia kuwa nilikuwa nimekamatwa kwa kuiba miraa ya muuguzi huyo. Waliniangusha chini kisha wakamwita mwanaume mwengine na wakasema wananifikisha katika kituo cha polisi cha Miccimikuru,” akasema Bw Muriira wakati wa mahojiano nyumbani kwake akiguguna kwa uchungu.

Badala ya kumpeleka kituoni umbali wa kilomita 3.5, walienda kwenye boma la muuguzi huyo.

“Alisema alitaka kunifundisha adabu na baada ya kuingizwa ndani ya nyumba alikuja na sindano na akadunga korodani yangu na kemikali yenye rangi nyekundu. Kutokana na uchungu nilipoteza fahamu,” akasema.

Alipopata fahamu, alijipata kituo cha polisi cha Muriira ambako alizuiliwa kwa siku mbili.

Licha ya kuwaambia polisi kuwa alikuwa amedungwa na dawa asiyoielewa, walikosa kuchukua hatua.

“Mmoja wao alinipiga kofi na kunirejesha kwenye seli. Niliachiliwa Jumapili baada ya mlalamishi kukosa kuendelea na mashtaka dhidi yangu,” akaongeza Bw Muriira.

Aliendea matibabu Hospitali ya Muthara lakini hali yake bado ipo tete. Sehemu zake nyeti zimefura na damu hutokea kwenye kidonda alikodungwa.

“Siwezi kulala usiku kwa sababu ya uchungu. Nasaka haki,” akasema.

Madaktari wa hospitalini walisema hawajafahamu kemikali ambayo Bw Muriira alidungwa nayo japo stakabadhi za matibabu zinaonyesha kuwa korodani yake imefura.

Mkuu wa Polisi wa Tigania ya Kati Florence Mbithe alisema kuwa Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) imemaliza uchunguzi na kuwasilisha faili kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP).

Bi Mbithe alisema washukiwa wawili wameandikisha taarifa pamoja na muuguzi ambaye alimdunga kwa kitu hicho.

“DCI imependekeza mshukiwa ashtakiwe kwa kusababisha majeraha mabaya, makosa ambayo husababisha adhabu ya kifungo cha maisha,” akasema.