Habari

Mwili waopolewa kutoka shimo la majitaka lililoporomoka watu wakitazama mechi

Na MISHI GONGO April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SIMANZI imegubika eneo la Kadzandani, Kaunti Ndogo ya Nyali, baada ya mwili wa mwanaume mmoja kuopolewa kutoka kwenye shimo la majitaka lililoporomoka Jumapili jioni.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mamlaka husika, mwili huo ndio wa pekee uliopatikana baada ya msako wa kina kufanywa na vikosi vya uokoaji.

Ajali hiyo ilitokea baada ya banda la video lililojengwa kinyume cha sheria juu ya shimo hilo lenye urefu wa futi 120 lilipoporomoka, wakati mechi ya kandanda ilipokuwa ikiendelea.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Mohamed Noor, alithibitisha kuwa mwili wa marehemu, Abdallah Aziz Abdallah, 54, uliopolewa mwendo wa saa 6:49 usiku wa kuamkia Jumatatu.

“Tumefaulu kuupata mwili wa Abdallah Aziz. Alitambuliwa na ndugu yake, Seif Aziz Abdallah, akiwa katika eneo la tukio,” alisema Bw Noor.

Mwanahabari akichukua video ya eneo ambako banda la video liliporomoka chini katika eneo la Kadzandani, Bamburi, Jumapili. Picha|Kevin Odit

Ripoti ya polisi ilieleza kuwa mguu wa kushoto wa marehemu ulikuwa umekatika, huenda kutokana na kifusi kilichomwangukia.

Mwili huo pamoja na mguu uliokatika ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Mafunzo ya Makadara.

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) eneo la Nyali anachunguza kisa hicho ambacho bado kinaendelea kuchunguzwa.

Dada yake marehemu, Mwanahamisi Aziz, alisimulia kwa huzuni jinsi alivyopokea taarifa hizo za kushtua.

“Ninaishi Utange. Rafiki yangu alinijia akisema kuna habari mbaya. Aliniambia shimo la majitaka limeanguka na kaka yangu ni miongoni mwa waliokuwa ndani,” alisema kwa masikitiko.

Mwanahamisi alisema marehemu alikuwa kondakta wa matatu eneo la Bamburi na ameacha mtoto mmoja.

Katika taarifa iliyotolewa na serikali ya Kaunti ya Mombasa siku ya Jumatatu, ilikisiwa kuwa watu wawili walikuwa wametumbukia.

Lakini baada ya kukamilika kwa zoezi la uokoaji ulipatikana mtu mmoja pekee.

Kisa hiki kimeibua maswali mazito kuhusu upangaji miji, utekelezaji wa usalama, na ujenzi holela katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu kaunti ya Mombasa.