Mwilu aponyoka kesi ya ufisadi, DPP aahidi rufaa
Na RICHARD MUNGUTI
NAIBU Jaji Mkuu Philomena Mbete Mwilu ameponyoka kesi ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Noordin Haji akaapa kuwasilisha malalamishi katika tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama (JSC).
Bw Haji alisema hayo alipohutubia wanahabari Ijumaa punde tu baada ya majaji watano wa Mahakama Kuu kufutilia mbali kesi aliyoshtakiwa Jaji Mwilu mbele ya hakimu mkuu Lawrence Mugambi mwaka uliopita.
“Tulitarajia kesi yetu inaweza kuzimwa lakini ushahidi tuko nao. Nitauwasilisha mbele ya JSC na kuomba achunguzwe sawia na kukata rufaa,” alisema Bw Haji.
Ijapokuwa majaji hao walizima hatua ya kumshtaki Jaji Mwilu pia walisema ushahidi ungewasilishwa mbele ya JSC achunguzwe na ikipatikana alikaidi maadili basi pendekezo litolewe kwa Rais ateue jopo la kumchunguza na hatimaye kutimuliwa kazini kwa utovu wa nidhamu.
Majaji Hellen Omondi, Francis Tuiyot, Mumbi Ngugi, William Musyoka na Enock Chacha Mwita waliosikiza ombi la Jaji Mwilu walisema kesi hiyo ilizinduliwa na DCI akitegemea ushahidi aliopata kwa njia isiyofaa.
Wakitamatisha kesi hiyo, majaji hao walisema DPP alitegemea ushahidi aliopata Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Geoffrey Kinoti alipochunguza akaunti ya benki ya kibinafsi ya Jaji Mwilu bila idhini.
“DCI alichunguza kimakosa akaunti ya kibinafsi ya Jaji Mwilu akitegemea agizo la mahakama ambalo halikuagiza akaunti ya kibinafsi ya Jaji Mwilu ichunguzwe,” walisema majaji hao watano.
Mashtaka yaliyomkabili yalidai alitumia mamlaka yake vibaya na kupokea mkopo wa Sh70 milioni kutoka kwa benki iliyofungwa ya Imperial Bank Limited (IBL) alipokuwa akihudumu katika Mahakama ya Rufaa.
Mahakama ilisema ushahidi uliopo ni kuwa Jaji Mwilu alimshawishi afisa mkuu wa IBL amruhusu (Jaji Mwilu) auze ardhi aliyokuwa ametumia kama dhamana aulipe mkopo huo.
“Hatujui ikiwa Jaji Mwilu alimshawishi afisa huyo wa benki kwa kutumia mamlaka ya afisi yake kama Jaji wa mahakama ya rufaa,” walisema majaji hao.
Haki
Majaji hao walisema hawakutamatisha kesi hiyo kwa vile haki za jaji huyo zilikandamizwa na DPP bali ni kwa sababu tabia ya DCI ambayo haiambatani na maadili mema.
Mahakama ilisema Jaji yeyote akitenda makosa akiwa kazini DPP na DCI wako huru kumtia nguvuni na kumshtaki huku wakisema aliyekuwa Jaji GBM Kariuki alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kujaribu kuua.
Mahakama ilisema Jaji Mwilu alishindwa kuwasilisha ushahidi kuwa alishtakiwa kama njia ya kulipiza kisasi kwa kutupa mbali matokeo ya kura za urais Agosti 2017.
Alikuwa amedai aliadhibiwa kwa uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya kura za urais.
Alisema kabla ya kushtakiwa maisha ya dereva wake yalitishwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Majaji walisema madai kuwa DCI hana mamlaka ya kuchunguza kesi za hujuma za kiuchumi hayana msingi kisheria.
Jaji Mwilu alikuwa amesema ni tume ya kupambana na ufisadi (EACC) tu ambayo ingelihoji jinsi alivyopewa mkopo huo na IBL.