Mwinjilisti kanisa la David Owuor adai amepandishwa cheo ili aondoe kesi
KESI dhidi ya uongozi wa Kanisa la Ministry of Repentance and Holiness linalohusishwa na Nabii Edward David Owuor kuhusu madai ya kuchafuliwa jina imechukua mkondo mpya, baada ya mlalamishi kudai Kanisa lilimpa cheo ili aondoe kesi.
Mwinjilisti Simon Aluchio ambaye amemshtaki Askofu Mkuu Jackson Barno wa tawi la kanisa hilo, Uasin Gishu, amekataa pendekezo la kumpa cheo cha askofu akilitaja kama jaribio la kumshawishi aondoe kesi ya kuharibiwa sifa.
Katika nakala zilizowasilishwa kortini baada ya mchakato wa kupatanisha pande hizo mbili kugonga mwamba, mhubiri huyo amedai alipatiwa wadhifa wa Askofu ili kumnyamazisha kuhusu suala hilo.
“Nimepandishwa cheo kuwa Askofu kupitia WhatsApp kunihadaa niondoe kesi, lakini kile tu ninaitisha ni kuombwa msamaha hadharani na Kanisa kupitia mtandao ule ule wa kijamii uliotumika kupaka tope jina langu,” alisema Bw Aluchio Jumanne baada ya kikao cha kusikiza kesi kuahirishwa.
Alisema picha akiwa na msimamizi wake mkuu mwanamke ilipigwa katika hospitali moja Eldoret walipozuru mgonjwa lakini ikasambazwa katika makundi mbalimbali ya kanisa hilo kumsawiri kama mkosa maadili kwa waumini wa kanisa hilo.
Bw Aluchio, ambaye ni kapera, amemshutumu askofu wake kwa kuchapisha madai yaliyomsawiri kama msherati na mtu mwovu na kusababisha afukuzwe kanisani.
Kesi hiyo ilipowasilishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Peter Ireri, Februari, askofu aliyeshtakiwa alielezea imani kwamba watasuluhisha tofauti zao kwa kuelewana na mlalamishi kwa ajili ya umoja na uwiano wa kanisa.
“Naomba korti hii itupatie nafasi ya kuridhiana kabla ya kwenda mchakato kamili wa kesi hii. Nina matumaini tutasuluhisha suala hili kupitia maelewano nje ya mahakama,” Askofu Barno alieleza korti.
Bw Aluchio, hata hivyo, anahoji askofu alichapisha maneno hayo ya kuchukiza Juni 5, 2024, mwendo wa saa 11:03 usiku kupitia nambari yake ya simu pasipo idhini kutoka kwake.
Anadai kitendo cha askofu kimemharibia sifa kama kiongozi wa kiroho na kutatiza fursa zake za kumpata mchumba ampendaye kutoka kanisa hilo.