MWISHO WA LAMI: Juhudi za Kombe kuokoa kiti chake zagonga mwamba kesi ikitupwa
MBUNGE wa Magarini Harrison Kombe amefikia kikomo katika juhudi za kutetea ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.
Hii ni baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali ombi lake la kuitaka ibatilishe uamuzi uliotolewa mwezi Mei na kuagiza alipe gharama zote za kesi.
Baada ya Mahakama ya Juu kukubaliana na maamuzi ya Mahakama Kuu na ile ya Rufaa, kwamba kulikuwa na udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi huo, Bw Kombe hakuridhika na alirudi katika korti hiyo ya upeo kuitaka itathmini upya uamuzi huo.
Sasa Mahakama ya Juu imeshikilia kwamba mbunge huyo wa chama cha ODM alipoteza kiti chake cha eneobunge na hivyo kura ipigwe tena.
Kulingana Bw Kombe, uamuzi wa kesi hiyo uliosomwa na Jaji Mkuu Bi Martha Koome ulimtaka amlipie Bw Stanley Kenga (UDA) gharama ya kesi.
“Kuhusu suala la gharama , tumeshawishika kwamba kesi hii ni kinyume cha sheria za mahakama na ni lazima mlalamishi abebe gharama ya kuileta hapa. Kwa hivyo, atalipia gharama zote,” akasema Jaji Mkuu katika uamuzi huo.
Kwa mujibu wa Bi Koome, mbunge huyo alisema mahakama hizo tatu ziliafikia maamuzi yao kwa misingi ya tafsiri mbaya ya ushahidi uliowasilishwa na mpinzani wake Bw Kenga.
Korti hizo tatu kwa pamoja zilithibitisha kwamba kulikuwa na udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi wa ubunge wa eneo la Magarini.
“Mahakama hii inapotoa uamuzi wake huwa tumemaliza jukumu letu kuhusiana na kesi. Hivyo, uamuzi huo utasalia ulivyo hadi utakapobadilishwa katika hali ya kipekee kama inavyoelezwa katika Aya ya 21A na 28(5) ya Sheria ya Mahakama ya Juu,” akaeleza Jaji Mkuu.Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula alitangaza kiti cha Magarini kuwa wazi kupitia ilani kwenye gazeti la serikali Mei 10.
Kufikia sasa, kampeni zinaendelea kati ya wanasiasa wanachama wa UDA na ODM. Chama cha Pamoja African Alliance kilicho ndani ya muungano wa Kenya Kwanza kilitangaza kwamba pia kitakuwa na mgombea wake debeni.
Bw Kenga alikuwa Mwakilishi wa Wadi ya Adu katika eneobunge la Magarini na Naibu Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi.Alishindwa kwa kura 21 baada ya kuzoa 11,925 huku Bw Kombe akizoa 11,946.
Bw Kenga alienda mahakamani kupinga ushindi wa bw Kombe.