Mzee arejea kwake nyumbani Gatundu Kaskazini baada ya kutoweka kwa miaka 35
Na LAWRENCE ONGARO
FAMILIA moja katika kijiji cha Mwea, Gatundu Kaskazini ilikuwa na furaha Jumanne hii ikiwa ni baada ya kurejea mwanamume mzee wa boma aliyetoweka miaka 35 iliyopita.
Mzee Lawrence Njuguna, 80, alipata mapokezi mazuri na kuibua kumbukumbu za mwana mpotevu katika Biblia.
Bw Njuguna alieleza kwamba alitoka nyumbani kwake mwaka wa 1986 na baadaye alijipata Kajiado ambako alianza kuuza makaa kwa muda wa miaka 20 kabla ya kuvuka mpaka hadi nchi jirani ya Tanzania.
“Tangu nilipotoka kwa boma langu, nilipoteza mawasiliano muhimu na watu wa familia na hadi wa sasa, sijawahi kuwa na simu ya rununu,” alisema mzee Njuguna.
Boma la mzee Njuguna lilikuwa mwenyeji wa kijiji chote cha Mwea ambapo wakazi walifurika kujionea wenyewe kama kweli ni yeye.
Alisema akiwa nchini Tanzania aliishi huko kwa zaidi ya miaka 10 akiendesha biashara ya kuuza mchanga.
Hata hivyo, alieleza kwamba maisha yalikuwa ya kujikaza tu.
Mkewe, Bi Mary Nyathira Njuguna, alionyesha uso wa furaha isiyo na kifani pamoja na familia yake kwa jumla wakati wanamkaribisha mzee huyo mwenye boma aliyesahaulika na wengi.
“Mimi sina ubaya wowote na mume wangu; namkaribisha kwa mikono miwili ili azidi kuwa na sisi kama familia. Tumemtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio,” alisema Bi Njuguna.
Afurahia familia pana
Mzee Njuguna alifurahia kupata familia ya watoto wanane na wajukuu kadha wakimkaribisha kwa furaha na shangwe.
“Nimefurahi kuona wajukuu wengi wakiwa hapa nyumbani na ni muda mrefu kweli tangu nitoke hapa bomani. Kweli Mungu ni mkubwa ,” alisema Bw Njuguna.
Alisema atalazimika kupumzisha akili kwanza ili afikirie ni jambo lipi atafanya baada ya kupotea kwa muda huo wote.
Kijana wake mkubwa Bw Samuel Irungu, alifurahi kumwona babake mzazi ambaye alitoweka akiwa mtoto na sasa ameoa na ana watoto.
“Sisi kama familia tunaona Mungu ametenda maajabu kwetu. Tumejaribu kufuatilia kwa muda mrefu ili kujua hasa baba yetu alikwenda wapi,” alisema Bw Irungu.
Tukio hilo la mzee huyo kurejea nyumbani baada ya muda mrefu limekuwa mjadala mkubwa katika kijiji chote cha Mwea na maeneo jirani.