Habari

Mzee kuhukumiwa kwa kumuibia mjane pensheni ya Sh750,000

Na RICHARD MUNGUTI August 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MZEE, 70 anasubiri kuhukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuibia mjane pensheni ya mumewe ya Sh752,000 miaka 12 iliyopita.

Mzee Ibrahim Kenyoru Bwana atahukumiwa Agosti 11, 2025 na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani Benmark Ekhubi.

Kenyoru alipatikana na hatia ya kumuibia Hellen Kemuma Matura Sh752,526 kati ya Machi 20, 2013 na Aprili 22,2016.

Hakimu Ekhubi alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kabisa Kenyoru akishirikiana na watu wengine, aliiba pensheni hiyo ya marehemu mumewe.

Kiongozi wa mashtaka Sonia Njoki alikuwa ameomba Kenyoru aadhibiwe vikali.

“Mjane Kemuma na watoto wake wanaishi maisha ya uchochole kutokana kitendo cha Kenyoru,” akasema Bi Njoki.

“Pesa hizi za pensheni ya mumewe Kemuma ndizo alitazamia kuzitumia kuwaelimisha watoto na kujikimu kimaisha.

“Sasa wanaandamwa na umaskini na hata hawawezi kujikimu kimaisha. Mjane huyu na mayatima wake wanaishi maisha ya ufukara ndiyo maana Kenyoru anastahili kuadhibiwa ipasavyo,” akaongeza.

Kenyoru alikuwa amemlilia hakimu akimsihi asimsukume gerezani kutokana nsa umri wake mkubwa.

“Umri wangu ni zaidi ya miaka 70. Najuta nilishawishika kumwibia mjane na naomba mahakama iniadhibu kupitia ulipaji wa faini ama kifungo cha nje,” akaomba.

Hakimu alisema atamwadhibu Kenyoru Agosti 11 2025 baada ya kutathmini ripoti ya afisa wa idara ya urekebishaji tabia.

Pia alisema atazigatia malilio ya mkongwe huyo.

Kenyoru alishtakiwsa kuiba pesa hizo kutoka idara ya kushughulikia malipo ya pensheni ya watumishi wa umma katika jengo la Bima House iliyoko barabara ya Harambee, Nairobi