Mzee Moi alivyoomba asamehewe 2002
Na PETER MBURU
WAKENYA Jumanne waliamkia habari za kufariki kwa Rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi, ambaye alikuwa rais wa pili wa Jamhuri ya Kenya kati ya 1978 na 2002.
Mzee Moi alifariki katika Nairobi Hospital akiwa na umri wa miaka 95.
Kulingana na mwanawe, Seneta Gideon Moi wa Baringo, Mzee Moi alikata roho jana alfajiri: “Mzee alifariki alfajiri mwendo wa saa kumi na moja na dakika ishirini. Alifariki kwa amani. Nilikuwa kando yake na kama familia tumekubali.”
katika hifadhi ya maiti ya Lee jijini Nairobi, shughuli zilikuwa nyingi kutwa nzima, huku viongozi wa kisiasa, kidini na na wa kijeshi wakifika humo kuutazama mwili wa Mzee Moi.
Mwili wake ulisafirishwa hadi mochari hiyo mwendo wa saa mbili asubuhi huku ulinzi katika hifadhi hiyo ya maiti ukiimarishwa na maafisa wa GSU.
Sehemu moja ya barabara ya Argwings Kodhek ambayo iko karibu na mochari hiyo ilifungwa kwa matumizi ya umma, ili kurahisisha shughuli nyingi zilizokuwa zikiendelea katika mochari hiyo.
Naibu Rais William Ruto alikuwa mmoja wa wanasiasa walioenda kuutazama mwili wa Mzee Moi.
Mwanawe Raymond Moi, ambaye ni Mbunge wa Rongai katika Kaunti ya Nakuru, alisema familia baadaye itatoa habari kamili kwa Wakenya kuhusu jinsi afya ya marehemu ilivyokuwa miezi michache iliyopita.
“Tunafahamu kuwa ujuzi wa juu zaidi kisayansi na dawa bora zilitumika kujaribu kuokoa maisha ya mzee, lakini Mungu alikuwa ameamua kuwa muda wake umefika,” akasema Raymond.
Rais Uhuru Kenyatta Jumanne alitangaza rasmi kuwa taifa litamuomboleza Mzee Moi hadi atakapozikwa ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti.
Katika utawala wake wa zaidi ya miongo miwili, Mzee Moi alipata wapenzi na wakosoaji wengi kutokana na mbinu alizotumia kuongoza.
Lakini atakumbukwa kuwa aliyefanya juhudi kuinua viwango vya elimu nchini kwa kujenga shule nyingi na kuzindua mradi wa kuwapa watoto maziwa shuleni, pamoja na kuhimiza umoja na amani.
Moja kati ya hotuba zake za mwisho alipokuwa akiondoka uongozini mnamo 2002 imegeuka kuwa bora zaidi alipoomba msamaha kwa wote aliowakosea.
“Wale wanaotaka kuongoza msiweke Kenya chini, msiweke msingi wa siasa zenu kwa chuki. Kama yuko mtu amenitukana namsamehe, na kama kuna mtu ambaye nimesema chochote kikaumiza roho yake anisamehe,” Mzee Moi akasema mnamo 2002.