Mzee wa mtaa jela miaka 20 kwa kupiga mwanamume aliyeomba chakula cha msaada
MZEE wa mtaa na mshirika wake watatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la kumshambulia mwenzao huku wakigombania chakula cha msaada.
Hii ni baada ya Mahakama ya Rufaa kukataa kupitia upya hukumu waliyopewa na mahakama ya hakimu.
Mohamed Baishe na mzee wa kijiji wa Kwasasi, Kaunti ya Lamu, Mohamed Shee, walipatikana na hatia ya kumshambulia Bw Yusuf Ali Sese kinyume cha sheria kuhusu unga wa mahindi.
Kisa hicho kilitokea wakati Bw Sese alipokuwa ameenda kuazima makaa ya kuwasha moto na akawakuta wawili hao wakiwa na pakiti za chakula cha msaada.
Majaji Agnes Murgor, Dkt Kibaya Laibuta, na Ngenye Macharia walikubaliana na maamuzi ya Mahakama ya Mahakimu na Mahakama Kuu kuwa washtakiwa walimvamia na kumjeruhi mwathiriwa.
“Tumeridhika kwamba washtakiwa walihukumiwa ipasavyo na mahakama ya mahakimu. Mahakama Kuu ilichambua upya ushahidi kwa makini na kufikia uamuzi wa haki. Tunakubaliana kwamba mahakama zote mbili zilifikia hitimisho sahihi kuhusu hatia ya washitakiwa,” majaji walisema katika uamuzi wao wa Januari 24, 2025.
Majaji hao walibainisha kuwa, kesi hiyo haionyeshi hali yoyote ambapo washtakiwa walichokozwa au walikuwa kwenye hatari ya kuumizwa na mwathiriwa.
“Tunasema hivi kwa sababu mwathiriwa alipofika nyumbani kwa Shee na kumkuta Baishe, jamaa huyo (Baishe) alianza ugomvi naye bila kuchokozwa. Baishe, bila kuchokozwa, alichukua panga na kuanza kumkata. Shee alimsaidia mshirika wake kutekeleza kitendo hicho cha kikatili kwa kumkamata mwathiriwa chini huku Baishe akiendelea kumkata,” majaji hao waliamua.
Majaji hao walitupilia mbali rufaa hiyo na kuthibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu, wakiamua kuwa wawili hao wanapaswa kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.
Baishe na Shee walishtakiwa kwa pamoja kwa kosa la kumsababishia Bw Sese madhara makubwa ya mwili.
Serikali ilisema wawili hao walitekeleza kosa hilo Aprili 30, 2020 katika eneo la Lamu Magharibi.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi wanane ambao walieleza kwa kina jinsi Baishe na Shee walivyomjeruhi vibaya Bw Sese.
Bw Sese alisema hapo awali alijaribu kushiriki karamu iliyokuwa ikiandaliwa na Baishe lakini alikataliwa.
Kisha akarudi nyumbani kwake ili kuandaa chakula chake mwenyewe. Alipokwenda nyumbani kwa Shee kuazima makaa ya kuwasha moto, alimkuta Baishe, ambaye alianza ugomvi naye.
Mzozo huo ulizidi kuwa mkubwa pale ambapo Baishe alimsukuma chini, akachukua panga kutoka ukutani, na kuanza kumshambulia.
Bw Sese alipojaribu kujikinga, alipata majeraha makubwa kwenye mikono, kichwa, na mabega yake.
“Sikuweza kutoroka kwa sababu Shee alinizingira kwa kunishika suruali, akinizuia nisiende popote,” Bw Sese alieleza mahakama.
Mahakama iliambiwa kuwa ni baada tu ya Bw Sese kuzimia kwa majeraha yake ndipo Shee alimwachilia kabla ya Baishe kutoroka.