Habari

Mzoga wa ndovu maarufu kuhifadhiwa katika makavazi ya kitaifa

Na STANLEY NGOTHO January 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MABAKI ya Craig, ndovu maarufu nchini Kenya aliyekuwa akitambulika kwa pembe zake kubwa zilizokuwa zikigusa ardhi na kuwa na uzito wa zaidi ya kilo 45, yataihifadhiwa katika Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.

Upasuaji uliofanywa na madaktari wa mifugo wa Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS) Jumamosi alasiri, ulionyesha kuwa ndovu huyo aliyekuwa akiishi katika Hifadhi ya Taifa ya Amboseli, Kaunti ya Kajiado, kwa zaidi ya miaka 50, alifariki kutokana na kujikunja kwa utumbo mkubwa.

Ndani ya saa 24 baada ya kifo cha ndovu huyo aliyekuwa akipigwa picha zaidi, wahifadhi wa mazingira kutoka kote duniani walituma jumbe za rambirambi, wakimwomboleza mnyama aliyetambuliwa kama kivutio kikubwa cha utalii katika mfumo wa ikolojia wa Amboseli.

Msaidizi wa Mkurugenzi wa Hifadhi ya Taifa ya Amboseli, Bw Paul Wambi, aliambia Taifa Dijitali kuwa mabadiliko ya lishe pamoja na uzee wa ndovu huyo yalisababisha tatizo hilo la kiafya.

“Kutokana na sababu zinazohusiana na uzee, tembo huyo alifariki kwa sababu ya kujikunja kwa utumbo mkubwa, hali iliyochangiwa na mabadiliko ya chakula,” alisema Bw Wambi.

Aliongeza kuwa KWS kwa kushirikiana na Makavazi ya Kitaifa ya Kenya imeamua kuandaa mabaki ya Craig ili kuhifadhiwa.

“Mabaki hayo yatatibiwa na kuhifadhiwa katika Makavazi ya Kitaifa ya Kenya kwa madhumuni ya kielimu, burudani na kuhamasisha vizazi vijavyo kuhusu uhifadhi,” aliongeza.

Craig atakuwa ndovu wa pili mashuhuri kutoka Amboseli kuhifadhiwa katika makavazi hayo baada ya tembo mwingine maarufu, Tim, aliyefariki mwaka 2020.