Habari

Nahangaishwa sababu ya kuambia serikali ukweli – Jayne Kihara

Na RICHARD MUNGUTI July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Naivasha Jayne Njeri Wanjiru Kihara ametifua kifumbi katika mahakama ya Nairobi akidai anadhulumiwa na kuteswa kisiasa kutokana na msimamo wake wa kusema jinsi mambo yalivyo nchini.

Akiomba hakimu mwandamizi Benmark Ekhubi asitishe kesi aliyoshtakiwa ya uchochezi, Bi Kihara kupitia mawakili Kalonzo Musyoka, C N Kihara, Edward Muriu (mbunge wa Gatanga), Daniel Maanzo (seneta Makueni) na Njiru Ndegwa alisema “kesi aliyoshtakiwa ni mbinu za kumfunga mdomo na ukiukaji wa hali ya juu wa haki zake za kikatiba.”

Mabw Musyoka, Kihara, Muriu na Ndegwa walimsihi hakimu asitishe kumsomea shtaka Bi Kihara hadi pale Mahakama kuu itakapotoa uamuzi ikiwa “mbunge anapasa kuwaeleza wapiga kura waliomchagua mambo yalivyo.”

Bw Ndegwa alisema Vifungu nambari 10 na Sheria namba 8 vya mamlaka ya mahakimu vimeipa korti uwezo wa kutathmini na kufafanua haki za kimsingi za kila Mkenya.

Bw Ndegwa alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga alipotoka katika kumshtaki Bi Kihara kwa kosa la uchochezi kwa kueleza wakazi wa Naivasha kwamba “majangili walisafirishwa kwa malori ya NYS  kutekeleza uhalifu uliopelekea mtu mmoja kuuawa mnamo Juni 25, 2025 wakati wa maandamano ya kupinga maongozi duni ya serikali.”

Mawakili hao walimsihi hakimu asiwe na kasi na pupa ya kumtaka Bi Kihara ajibu kesi aliyoshtakiwa ndipo Mahakama Kuu itathmini vipengee kuhusu uhuru wa kuzungumza.

Hakimu huyo aliombwa asitishe kwa siku 14 kumwezesha Bi Kihara kuwasilisha kesi katika Mahakama kuu kupata maelezo ikiwa “kama Mbunge wa Naivasha ikiwa anapasa kuwafafanulia wapiga taswira ya jinsi mambo yalivyo ama anapasa kunyamaza na kutulia tulii kana kwamba mambo ni barabara na kumbe yameharibika.”

Ombi hilo la kusitishwa kwa kesi dhidi ya Mbunge huyo ilipingwa vikali na kiongozi wa mashtaka Norah Awiti akisema “shtaka dhidi ya Kihara linaambatana na vipengee vya kisheria.”

Bi Awiti alisema mahakama iko na uwezo wa kung’amua uhakiki wa kisheria na ushahidi utakaowasilishwa.

Bw Ekhubi atatoa uamuzi Agosti 7, 2025 ikiwa atasitisha kesi hiyo hadi Mahakama kuu itakapotoa mwelekeo au la.

Bi Kihara yuko nje na dhamana ya Sh50,000.