Nairobi, Kiambu, Mombasa hazilipi wanakandarasi, Ripoti yaonyesha
KAUNTI za Nairobi, Kiambu na Mombasa ni kati ya saba ambazo wawasilishaji bidhaa na wanakandarasi hawalipwi, wakiwa na madeni ya zaidi ya miaka mitatu.
Ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti Dkt Margaret Nyakang’o imeanika kaunti hizo tatu na nyingine nne ambako waliowasilisha bidhaa na wanakandarasi hawajalipwa kwa muda wa miaka mitatu.
Kaunti nyingine ambako waliotoa huduma kwa kaunti hawajalipwa kwa zaidi ya miaka mitatu ni Machakos, Wajir, Nakuru na Bungoma.
Wanakandarasi na wawasilishaji bidhaa wamekuwa wakilalamika malipo kuchelewa, hali hiyo ikisababisha baadhi ya watu kukatiza uhai wao kupitia kitanzi, wengine wakiandamwa na maradhi kutokana na msongo wa mawazo.
Baadhi huishia kusambaratika kabisa kimaisha biashara zao zikiandamwa na benki na asasi nyingine zilizowakopa pesa.
Kwa upande mwingine, Baringo, Elgeyo Marakwet, Kericho, Lamu, Makueni, Nandi, Turkana na Pokot Magharibi ni kaunti ambazo huwalipa wawasilishaji bidhaa kwa wakati na hazina madeni ambayo yanapita miaka miwili.
Ripoti hiyo ilifichua kuwa madeni ambayo yamepita miaka mitatu yanajumuisha zaidi ya nusu ya madeni yote ya Sh176.8 bilioni ambapo ni Sh85.4 bilioni.
Utawala wa Gavana Johnson Sakaja ndio uko pabaya zaidi baada ya kukosa kuwalipa wanakandarasi na wawasilishaji bidhaa jumla ya Sh62.38 bilioni kwa muda wa miaka mitatu.
Licha ya kuzongwa na madeni kibao, Nairobi inaendelea kuyarundika madeni mengine na mwaka jana pekee inadaiwa Sh12.6 bilioni.
Gavana Sakaja anaonekana kuzoea madeni kwa kuwa hajalipa hata wanakandarasi wapya waliotoa huduma kwa kaunti ambapo deni hilo limepanda hadi Sh777.8 milioni kwa muda wa mwaka mmoja.
Kaunti jirani ya Kiambu pia ni mahangaiko matupu kwa wawasilishaji bidhaa na wanaotoa huduma kwa kaunti.
Utawala wa Gavana Kimani Wamatangi haujalipa Sh3.8 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu. Katika mwaka mmoja, utawala huo unadaiwa Sh2.27 bilioni na waliofanya kazi na kaunti.
Kati ya deni la Sh3.86 bilioni ambalo Mombasa linadaiwa, Sh3 bilioni hazijalipwa wakati wa utawala wa miaka mitatu ya Gavana Abdulswamad Nassir.
Gavana Wavinya Ndeti anapambana kwa kutowalipa wawasilishaji bidhaa Sh6.73 bilioni kisha wanakandarasi Sh2.3 bilioni, deni ambalo limedumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Machakos pia imerundika deni la Sh2.56 bilioni kwa muda wa mwaka mmoja licha ya kuandamwa na madeni chungu nzima ya zamani.
Licha ya zaidi ya theluthi ya madeni ya Sh3.6 bilioni ya Bungoma yamedumu kwa zaidi ya miaka mitatu (Sh1.09 bilioni), kaunti haionekani kujishughulisha na hilo ambapo imerundika Sh1.62 bilioni kwa mwaka.
Wajir ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG) Ahmed Abdullahi ina deni la Sh3.7 bilioni ambapo Sh1.65 bilioni hazijalipwa kwa miaka mitatu.
Ndani ya mwaka mmoja pekee kaunti hiyo imerundika deni la Sh2 bilioni.