Habari

Naomba radhi kupiga ‘Ndio’ kwenye mswada, mbunge wa Taveta sasa arai wakazi

June 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Taveta, John Bwire, ameomba msamaha wakazi wa Taveta kwa kuunga mkono mswada wa fedha uliokuwa na utata. 

Bw Bwire, ambaye alipiga kura ya “ndio” kwenye mswada huo, alisema alikosea wapiga kura wa eneo hilo kwa kuunga mkono na hivyo kulazimika kuomba msamaha.

“Duniani hakuna aliye mkamilifu. Naombeni msamaha nilikosea kwa kupiga “Ndio”. Nimejifunza kitu, ukikosea la muhimu ni kuomba msamaha, unavyoendelea kujieleza ndio unavyoendelea kukwaza uliowakosea,” aliandika kwa mtandao wake wa Facebook.

“Duniani hakuna aliye mkamilifu. Poleni sana. Maisha ni shule na kila siku naendelea kujifunza. Kwa hili nimejifunza,” aliandika.

Kauli yake imepokelewa kwa hisia tofauti na wananchi wa eneo hilo ambao walidai kuwa mbunge huyo hakutilia maanani maoni yao.

Mnamo Jumanne wiki hii, Bw Bwire hakufika bungeni wakati bunge hilo lilipokuwa likipitisha marekebisho ya mswada huo wa fedha wa mwaka 2024.

Haikubainika kwa nini mbunge huyo alikosa kufika. Wiki jana, alikemewa kwa kuidhinisha sheria hiyo wakati wa hatua ya pili ya usomaji.

Mswada huo ambao ulihusu masuala ya bajeti na matumizi ya serikali, uliaminika kuwa na athari kubwa kwa wananchi kwa sababu ya ushuru mpya.

Wiki jana, Bw Bwire alisema kuwa aliamua kuunga mkono mswada huo, akiamini kuwa serikali ina nia njema na inalenga kuboresha maisha ya wananchi huku akitaja lengo la ujenzi wa barabara mbili katika eneo la Taveta.

Vilevile, alikuwa amesema kuwa atatetea uamuzi wake akisema wananchi wake wangepata manufaa haswa kwa ujenzi wa barabara hizo za takriban Sh3.2 bilioni.

Hata hivyo, wananchi wa eneo hilo wamepokea kauli ya mbunge huyo kwa hisia tofauti huku baadhi wakimpongeza kwa kuwa mwaminifu na kujitolea kujifunza, na wengine kuhoji uhalali wa kauli yake.

Katika kaunti ya Taita Taveta wakati wa kupitishwa kwa marekebisho ya sheria hiyo, wabunge Lydia Haika (mwakilishi wa wanawake) na Peter Shake (Mwatate) waliyaunga mkono, huku Danson Mwashako (Wundanyi) na Abdi Chome (Voi) wakiyapinga.

Wakati wa maandamano ya Jumanne, maandamano yalishuhudiwa mjini Taveta na Voi ambapo waandamanaji waliwataka viongozi hao watatu kujiuzulu kwa kusaliti wananchi wa eneo hilo.

Mjini Voi, polisi walilazimika kupiga doria katika duka la jumla la mbunge Shake ili kuzuia njama zozote za uvamizi