Nassir ashutumu Ruto kwa kukalia fedha za ujenzi wa barabara mashinani
GAVANA wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir ameshutumu serikali ya kitaifa kwa kukalia fedha muhimu za ujenzi wa barabara huku muundomsingi wa kaunti ukisambaratika kutokana na uhaba wa pesa.
Bw Nassir amesema si haki kwa maafisa walioketi Nairobi ambao hawajui mahitaji ya raia mashinani kudhibiti mabilioni yaliyotengwa kwa ukarabati wa barabara za nyanjani.
Malalamishi ya gavana yanajiri wakati ambapo kumechipuka upya malumbano baina ya Rais William Ruto na magavana kuhusu usimamizi wa fedha za ukarabati wa barabara (RMLF).
Rais Ruto ametaka magavana waache kusukuma kusimamia pesa hizo akisema ni vyema serikali ya kitaifa kuendelea kuzigawa na kutuma moja kwa moja.
Ni msimamo ambao unamweka katika mgongano na mshirika wake katika Serikali Jumuishi Raila Odinga, ambaye amesisitiza kwamba ukarabati wa barabara za nyanjani umegatuliwa na hivyo basi fedha hizo zafaa ziwe mikononi mwa magavana.
Kaunti ya Mombasa inakabiliwa na barabara mbovu baada ya mvua kubwa kutokana na mfumo mbovu wa upitishaji majitaka na mashimo barabarani.
“Kwa nini serikali kuu ikatalie na pesa? Inakuwaje kwamba mtu ambaye hajui Mombasa anaamua jinsi pesa zitatumiwa,” akauliza.
Alilalamika kwamba magavana hulaumiwa kwa barabara mbovu kwenye gatuzi lao ilhali halmashauri zilizopewa jukumu la kukarabati barabara kama KeNHA na KURA hazielekezewi lawama.
“Sisi ndio tunajua kiatu kinatubana wapi,” akasema.