Nassir: Niligutushwa na simu ya Raila kwamba hafla ya ODM imeahirishwa
GAVANA wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, amefichua kuwa maadhimisho ya miaka 20 ya chama cha ODM, yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu, yaliahirishwa baada ya kupokea simu iliyomuita jijini Nairobi.
Akizungumza katika kikao na wajumbe wa chama hicho eneo la Mvita, Bw Nassir alieleza jinsi alivyopokea simu ya ghafla ikimtaka afike Nairobi kwa mashauriano ya dharura na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.
Gavana huyo alisema simu hiyo ilimshangaza kwani maandalizi ya sherehe hizo Mombasa yalikuwa yamekamilika.
“Niliarifiwa kuwa Raila ananiita Nairobi. Nilipokagua ratiba, nilibaini kuwa singefika kwa wakati, hivyo wakanielekeza nijiunge kupitia Zoom. Unajua, ukiambiwa jambo na Raila, lazima utafakari sana na utashindwa utasema nini,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw Nassir, Bw Odinga alieleza kuwa baadhi ya kaunti bado hazijafanya maadhimisho yao ya miaka 20 ya ODM, na kwamba kuendelea na sherehe za Mombasa kama ilivyopangwa kungeathiri shughuli za maeneo mengine.
“Hapa Mombasa tulikuwa tumejiandaa kikamilifu kwa maadhimisho hayo, lakini Raila aliniambia kuwa baadhi ya wenzangu kutoka maeneo kama Kajiado, Turkana na Nairobi bado hawajafanya yao. Akasema tukiyafanya sisi, hakuna mtu angependa kufuatilia yale ya wenzetu hata kwenye televisheni,” aliwaeleza wajumbe.
Kwa unyenyekevu, alisema viongozi wa Mombasa walikubali kuahirisha sherehe hizo ili kuruhusu maeneo mengine kufanya maadhimisho yao kwanza.
“Kwa shingo upande tulikubaliana kuahirisha sherehe zetu. Uamuzi huo ulifanyika kwa roho ya umoja na haki ndani ya chama,” alisema gavana huyo.
Bw Nassir amekuwa akikutana na wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya kaunti kujiandaa kwa hafla hiyo.
Wiki iliyopita, chama hicho kilitangaza kupitia taarifa kwamba maadhimisho ya Mombasa sasa yatafanyika kuanzia Novemba 14 hadi 16.
Chama hicho kilieleza kuwa, uamuzi wa kuahirisha hafla hiyo ulifikiwa baada ya kikao cha mashauriano na viongozi wake wa ngazi za juu. ODM ilibainisha kuwa bado kuna maombi kutoka kaunti ambazo viongozi hawajazuru katika mfululizo wa maadhimisho hayo.
Tayari chama hicho kimefanikiwa kufanya maadhimisho katika kaunti za Busia, Wajir, Kisii na Narok.
“Hata hivyo, bado kuna wito mkubwa kutoka maeneo mengine nchini kutaka tupeleke maadhimisho haya ya kihistoria huko pia, ili wale wasioweza kufika Mombasa wapate kushiriki,” chama hicho kilisema katika taarifa.
ODM ilisema hatua hiyo inalenga kupanua mpangilio wa maadhimisho hayo na kuhakikisha ushirikishwaji kabla ya kufanyika kwa sherehe kuu jijini Mombasa.
Hata hivyo, Bw Nassir alitangaza kuwa licha ya kuahirishwa kwa hafla hiyo, kaunti imeratibu shughuli kadhaa za utangulizi, ikiwamo mashindano ya kandanda yatakayofanyika Oktoba 9 na 10 yakihusisha timu nne — Shabana, Gor Mahia, Bandari na timu ya ODM.
Gavana Nassir aliwahakikishia wakazi wa Mombasa kuwa atatekeleza ahadi zake za kampeni kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.