Habari

Natembeya arushia makombora serikali, akiilaumu kwa ‘utekelezaji mbovu’ wa CBC

Na OSBORN MANYENGO January 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Kaunti ya Trans Nzoia, George Natembeya, ameibua wasiwasi mkubwa kuhusu Mtaala wa Umilisi, maarufu kama CBC, akitoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya dharura ili kushughulikia changamoto zake.

Gavana huyo ameonya kuwa masuala ambayo hayajatatuliwa kwenye mfumo wa elimu yanahatarisha mustakabali wa watoto wa Kenya.

“Wakenya wenzangu, hebu tuwe na mjadala wa kikweli kuhusu mtaala wa CBC. Je, kweli tunaandaa watoto wetu kwa maisha ya usoni au tunawahatarishia? Muda umefika tuwazie. Watoto wetu wanastahili mustakabali bora,” akasema.

Alikuwa akihutubia waombolezaji Alhamisi mjini Kitale wakati wa mazishi ya Askofu mstaafu Stephen Wamuti Njuguna wa Kanisa la Kenya Assemblies of God.

Gavana Natembeya alibainisha mapengo makubwa kwenye utekelezaji wa mtaala wa CBC ambayo, kwa maoni yake, lazima yashughulikiwe ili kufanikisha mfumo huo.

Aidha, Gavana Natembeya alikosoa baadhi ya usimamizi wa shule kwa kutoza ada za ziada kinyume na mwongozo wa serikali kuu.