Naugua kisukari na shinikizo la damu, Waititu alia akiomba korti imwachilie kwa dhamana
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ameomba korti imwachilie kwa dhamana akisubiri kusikilizwa kwa rufaa yake dhidi ya kifungo cha miaka 12 jela aliyopewa Alhamisi.
Katika ombi lake, Bw Waititu ametaja hali yake ya afya, madai ya dosari katika uamuzi wa jaji, majukumu ya kifamilia na uzito wa rufaa yake akiomba apewe dhamana.
Alihukumiwa kifungo cha miaka 12 gerezani ama alipe faini ya Sh53.5 kwa kupokea Sh25.6 kutoka kwa mkandarasi wa barabara aliyepewa zabuni ya Sh588 milioni na serikali ya Kaunti ya Kiambu.
Kulingana na Bw Waititu, uamuzi wa korti ulikuwa na mushkil kwa sababu ushahidi uliotolewa “ulikosa kuthibitisha kikamilifu kuwa alitekeleza kosa hilo.”
Aliongeza kuwa alihukumiwa kwa msingi wa shuhuda zilizokinzana na kuwa jaji aliamua visivyo kuwa alihusika na uhalifu kwa kufuata mkondo wa jinsi pesa hizo zilisambazwa.
Kwa hivyo, anataka korti itupilie mbali uamuzi wa kurasa 212 uliotolewa na Hakimu Mkuu Thomas Nzioki.
“Kwa kutoridhishwa na hukumu, Bw Waititu anataka kuwasilisha rufaa ambayo anaamini kuwa ina nafasi kubwa ya kufaulu. Ana hofu kuwa kesi hii inaweza kusikilizwa kwa muda na atakuwa ameanza kutumikia kifungo, hali ambayo itakiuka haki zake ikiwa rufaa itafaulu,” akasema wakili Danstan Omari.
Bw Omari anaomba ombi hilo lishughulikiwe kwa dharura akisema Bw Waititu hatawatisha mashahidi kwa sababu kesi hiyo iko katika mahakama ya rufaa.
Akikosoa uamuzi wa mahakama ya chini, wakili huyo anadai hakimu alikosa kutilia maanani ushahidi wa Bw Waititu na hakuupima dhidi ya ule wa upande wa mashtaka katika kufanya uamuzi wa haki.
Kuhusu afya ya kibinafsi, Bw Waititu amefichua kortini kupitia hati ya kiapo kwamba anakabiliwa na mseto wa magonjwa ya shinikizo ya damu na ugonjwa wa sukari.
“Ni hali ya kiafya ambayo inanilazimu kuchukua tahadhari maalum na matibabu ya kila mara kwani ni hali ambazo zinaweza kudhibitiwa tu lakini hazitibiki,” akasema Bw Waititu.
Pia alisema yeye ndiye tegemeo la kipekee la familia yake. Kwa hivyo, kuwa rumande akisubiri kusikilizwa kwa uamuzi wa rufaa hiyo kutaiacha familia yake ikitaabika, hali ya kukata tamaa na maisha yao yataathiriwa pakubwa.
Wakati wa kesi hiyo, aliiambia mahakama kuwa alikuwa mfanyabiashara anayejihusisha na ardhi.
Alikuwa nje kwa dhamana ya Sh30 milioni wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo. Sasa anaomba Mahakama Kuu ikubali dhamana hiyo hiyo ili awe huru.
Anaeleza kuwa dhamana iliyowekwa katika mahakama ya chini sasa ina thamani ya Sh50 milioni, ambayo ni sawa na faini aliyotozwa.