Ndege ya kwanza ya KQ kuashiria kurejelewa safari za ndege nchini yatua Kisumu
ELIZABETH OJINA na SAMMY WAWERU
NDEGE ya kwanza ya shirika la Kenya Airways (KQ) ya kuashiria kurejelewa safari za ndege nchini tangu ziyumbishwe na janga la Covid-19 imetua Kisumu ikiwa na abiria 66 saa tano na dakika ishirini.
Ndege hiyo KQ 655 ilikuwa ikitoka jijini Nairobi na imetua salama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu.
Miongoni mwa waliosafiri ni wadau muhimu katika sekta ya utalii na wafanyakazi wa Kaunti ya Kisumu na wale wa Mamlaka ya Viwanja Ndege Nchini (KAA).
Imetua ikiwa ni siku ya 99 tangu ndege ya mwisho kutua katika uwanja huo wa Kisumu.
Ni afueni kwa wasafiri wanaotegemea safari za ndege. Kando na KQ, Jambojet nao wamerejesha safari hizo.
Wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kulegeza masharti yaliyowekwa kama hatua za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Kando na kuondoa zuio la kuingia na kutoka nje ya kaunti ya Nairobi, Mombasa na ile ya Mandera, na pia kuruhusu maeneo ya kuabudu kufunguliwa kwa awamu, kiongozi wa nchi alisema usafiri wa ndege nchini ungerejelewa leo Julai 15, 2020.
Rais Kenyatta pia alitangaza kwamba usafiri wa ndege nje ya nchi utaanza Agosti 1, 2020. Usafirishaji wa mizigo ndani na nje umekuwa ukiendelea.
Waziri wa Uchukuzi James Macharia mapema Jumatano katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Nairobi, ameongoza kuruhusu ndege ya kwanza kurejelea shughuli za usafiri ndani ya nchi.
Ndege zinazomilikiwa na shirika la KQ zimefungua jamvi la safari; moja ikielekea mjini Mombasa nayo nyingine ikielekea mjini Kisumu.
Waziri Macharia amesema hatua hiyo itasaidia kufufua biashara ya usafiri wa ndege, ambayo imeathirika kwa kiasi kikuu na Covid-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.
“Baada ya usafiri wa ndani kwa ndani kurejelewa, sasa tunalenga safari za kuingia ndani na kutoka nje. Zitaanza Agosti 1, 2020, na raia wetu wengi hasa waliofugiwa katika nchi za kigeni wana hamu kurejea nchini,” Bw Macharia ameeleza.
Ugonjwa wa Covid-19, ambao sasa ni janga la kimataifa umeathiri uchumi wa nchi na sekta mbalimbali, ikiwemo kufifisha uchumi na kuyumbisha biashara na pia watu kupoteza ajira.
Kisa cha kwanza cha Covid-19 kilithibitishwa nchini Machi 13, 2020.