Habari

Ndege yaanguka na kuua watu wanne Mwihoko

Na SIMON CIURI August 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NDEGE ndogo ya Shirika la Matibabu na Utafiti la Afrika (AMREF) ilianguka na kulipuka katika eneo la makazi Mwihoko, Kaunti ya Kiambu.

Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa nane na dakika 35 mchana, karibu na kituo cha biashara Mwihoko, katika mpaka wa kaunti za Kiambu na Nairobi.

Kwa mujibu wa ripoti za polisi, watu wanne waliokuwa ndani ya ndege hiyo walifariki dunia papo hapo.

Wawili zaidi, ambao ni wakazi wa eneo hilo, walijeruhiwa baada ya ndege hiyo kuangukia nyumba zao ilipokuwa ikijaribu kutua kwa dharura.

Ndege hiyo, ambayo ilikuwa ikiruka juu ya eneo hilo, ilianguka na kulipuka mara moja, na kusababisha hofu miongoni mwa wakazi.

Baada ya ajali, wakazi walikimbilia eneo la tukio na kuanza juhudi za uokoaji kabla ya maafisa wa usalama kufika.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (KCAA) haikuwa imetoa taarifa rasmi kufikia wakati wa kuchapisha habari hizi kuhusu umiliki wa ndege hiyo, japo taarifa za awali zinaashiria kuwa ilikuwa ya AMREF.

Kwa sasa, vikosi vya usalama kutoka kaunti za Kiambu na Nairobi vipo katika eneo hilo vikiratibu shughuli za uokoaji, kuondoa mabaki ya ndege, na kuhakikisha usalama.

Wakazi wametakiwa kuendelea kuwa watulivu huku uchunguzi kamili ukiendelea kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo ya kusikitisha.