Habari

Ndege yakwama kwenye tope Mandera

October 21st, 2019 1 min read

Na MANASE OTSIALO

NDEGE moja ya Rudufu Air humu nchini, imekwama kwenye tope katika uwanja mdogo wa ndege wa Takaba, Mandera Magharibi baada ya kuteleza kutoka kwa njia yake yake wakati ikitaka kupaa Jumapili.

Mfanyakazi wa Khadija Buko, asasi inayojishughulisha na ukataji wa tiketi, ameambia Taifa Leo kwamba kwa siku ya pili sasa, ndege hiyo bado kuondolewa kwenye tope hilo; ikiwa ni siku ya pili.

“Ndege hiyo ilikuwa na abiria 30 wakati wa mkasa huo. Kwa sasa wangali salama mjini Takaba,” amesema mfanyakazi huyo ambaye hana ruhusa ya kuzungumza na vyombo vya habari akiongeza kwamba walijaribu kuivuta ndege hiyo kwa kutumia lori la polisi bila mafanikio.

Mafuriko yanayosababishwa na mvua nyingi yanatatiza juhudi za kuiondoa ndege hiyo kwenye tope.

“Ama tutasubiri matope yakauke au tusubiri tupate trekta la kuivuta ndege kutoka matopeni, amesema.

Ndege hiyo iliteleza kutoka kwa njia yake katika uwanja huo Jumapili mchana ikitaka kupaa kuelekea mjini Mandera.

Rudufu Air yenye afisi zake katika Uwanja wa Ndege wa Wilson ina ndege za mkondo wa Nairobi-Takaba-Mandera.

Naibu Kamishna wa Mandera Magharibi Kipkoech Labatt amethibitisha kutokea kwa mkasa huo.

“Tunatafuta trekta,” amesema Bw Labatt.

Wakati wa sherehe za Mashujaa Dei, Gavana wa Mandera Ali Roba amesema uwanja wa ndege wa Takaba utazungushwa ua kasha ufanyiwe ukarabati katika kipindi kijacho cha muda wa miezi mitatu.

Mapema mwaka 2019, wakazi wa eneo hilo walikuwa wameonyesha pingamizi za kujengwa kwa uwanja huo wakisema watapoteza eneo kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.