Habari

Ndindi Nyoro amuonya Ruto kuhusu kukopa zaidi huko Uchina

Na MARTIN MWAURA April 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro amemwonya Rais William Ruto dhidi ya kuendelea kukopa akisema kuwa hatua hiyo itasababisha janga la kiuchumi nchini.

Bw Nyoro alisema Kenya lazima iangazie njia ya kudhibiti madeni yake huku akisisitiza kuwa kopakopa zisizokwisha ni tishio kwa uchumi wa nchi.

Aliongeza kuwa Kenya ina rasilimali za kutosha na kuna njia nyingi ya kupata pesa za kugharimia miradi ya maendeleo badala ya kukopa.

Kufikia Machi 2025, deni la Kenya lilikuwa limegonga Sh11.02 trilioni kutoka Sh10.5 trilioni kufikia Juni 2024.

“Nilitoa taarifa kuhusu kiwango cha deni la taifa na watu hasa wale ambao wanafanya uamuzi nchini walijitetea. Tukiibua suala la kitaifa watu hawafai kujitetea bali walizungumzie kwa sababu sote tunaangazia mustakabali wa kiuchumi wa nchi yetu,” akasema Bw Nyoro.

Mbunge huyo Kiharu alisema hayo wakati Rais William Ruto anaendelea na ziara yake Beijing China. Jana, Rais alishuhudia kutiwa saini kwa mkataba wa Sh107 bilioni na kampuni saba za China.

Kampuni hizo ni za utengenezaji wa bidhaa, kilimo, utalii, teknolojia na zinalenga kubuni nafasi ya ajira kwa vijana pamoja na kusaidia uchumi kukua kwa mujibu wa Rais Ruto.