Ndoto yangu imetimia, asema Ruto akipeana nyumba 1,080 za bei nafuu Mukuru
NYUMBA za kwanza chini ya mradi ya Nyumba Nafuu wa Rais William Ruto sasa zimechukuliwa na kutoa sura mpya kwa wakazi wa mtaa wa mabanda jijini Nairobi.
Nyumba hizo 1,080 katika mtaa wa Mukuru zilipewa wamiliki katika hafla ya kufana ambayo Rais alipeana funguo na kuwatakia maisha mema wanapoanza safari ya kumiliki rasilmali jijini Nairobi.
Nataka kuwaambia wakazi wa Mukuru, mna furaha lakini mimi hata ndio nina furaha zaidi kwa sababu ndoto yangu imetimia. Ndoto ya kuinua maisha ya watu wa chini, niwaweke juu. Hii ndio siku muhimu zaidi katika maisha yangu ya kisiasa — Rais Ruto

Wengi wa walionufaika na nyumba hizo wamekuwa wakiishi katika mabanda ya mabati kwenye kitongoji duni cha Mukuru na Mariguini, na hawakuficha furaha yao kubadilishiwa maeneo ya makazi.
Richard Mauko, 45, ambaye amekuwa akiishi katika mtaa wa Mukuru kwa Njenga huku akilipa kodi ya Sh2,500 asema kujipatia nyumba ya aina ya bedsitter kwenye mazingira ya hadhi kama yale ni ufanisi mkubwa kwake.
“Nina familia ya watoto wawili na huu ni ufanisi mkubwa kwangu. Hizi si tetesi tena, sasa ninamiliki nyumba iliyo na maji, choo, stima na gesi ya kupikia Nairobi,” akasema Bw Mauko.
Serikali ilikuwa imesema kwamba wakazi wa Mukuru na Mariguini watapewa kipau mbele katika kugawanya nyumba hizo pindi zitakapokamilika.
Mauko anafichua kwamba amekuta nyumba hiyo ikiwa na kitanda cha double decker, godoro la maana, jambo alilosema limemfurahisha pakubwa.

“Tayari nina kitanda na kochi. Niko sawa kabisa. Kilichobakia ni kwenda kuchukua familia yangu na vifaa vingine vichache. Nitalala hapa leo,” akasema akiwa na furaha kubwa.
Jacinta Regere kutoka Mariguini pia alipokea funguo ya nyumba yake mpya.
Asema imekuja wakati mwafaka zaidi kwa sababu amekuwa akipambana na mafuriko kwenye mtaa wa mabanda wakati huu wa mvua kubwa.
“Mafuriko yalikuwa yanajaa kwangu na nilipoteza stakabadhi zangu muhimu. Tunamshukuru Mungu kwa sababu ya Rais. Kila kunaponyesha kwenye mtaa wa mabanda, unatumia muda wote kufagia maji usiku na mchana,” akasema Bi Jacinta.
Anaonekana kufurahia zaidi mfereji wa kuoga (shower) ulioko ndani ya nyumba yake, gesi ya kupikia pamoja na usalama uliopo kwenye makazi mapya, jambo analosema hajawahi kupata katika miaka 20 aliyoishi jijini.
Ni hisia ambazo zimesheheni kwa mamia ya wakazi waliopokezwa nyumba mpya na serikali.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Nyumba Nafuu Sheila Waweru, nyumba zote zipo wazi kuchukuliwa kupitia kwa mpango wa ulipaji wa muda mrefu ambao unaruhusu wanunuzi kulipia kwa viwango vidogo kwa muda wa miaka 30.