Ni juu yenu kuamua hatima ya SHA, Gathungu aambia Wabunge
MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu amewaambia wabunge kwamba ni juu yao kuamua iwapo watasitisha mfumo tata wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) uliogharimu Sh104.8 bilioni baada ya ofisi yake kufichua uozo kuhusu kandarasi iliyotumiwa kuunua.
Haya yanajiri baada ya wabunge hao kumuuliza Bi Gathungu kwa nini alikosa kupendekeza kusitishwa kwa mfumo wa Teknolojia ya Habari za Afya (IHTS) unaotiliwa shaka.
Hii ni baada ya mkaguzi huyo kutoa ripoti iliyokosa mfumo huo, na kuibua wasiwasi mkubwa kuhusu uamuzi wa serikali kuendelea na mradi huo.
Mfumo huo ni miundombinu muhimu ya utekelezaji wa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF), iliyochukua nafasi ya Hazina ya Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Umma ya Jumanne, maseneta walimbana Bi Gathungu wakimuuliza kwa nini hakupendekeza kushtakiwa kwa maafisa wa Serikali waliohusika katika kashfa hiyo pamoja na kufichua majina yao.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alitoa wito wa kusitishwa kwa kandarasi hiyo, akisema nchi haiwezi kuendelea kutumia mfumo ambao ulipatikana kwa uhalifu.
Alimuuliza mkaguzi mkuu ni nini kinamzuia kutoa mapendekezo kama vile kufunguliwa mashtaka kwa waliohusika katika sakata hiyo, akisema jinsi ilivyo, ripoti hiyo haina matokeo halisi.
“Mapendekezo yalipaswa kuwa na matokeo halisi kwa maafisa waliokiuka sheria,” alisema Seneta Sifuna.
“Inaonekana watu pekee ambao mfumo unawafanyia kazi ni wale wanaopata hongo. Tunapaswa kuukomesha na kukabiliana na matokeo yake baadaye,” akaongeza Katibu Mkuu wa chama cha ODM.
Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ aliongeza kuwa SHA imegeuka kuwa chombo maalum cha kupora rasilimali za umma.
Alisema kuwa nchi inahitaji kujua watu binafsi waliohusika katika mchakato wa ununuzi.
Hata hivyo, Bi Gathungu alisema tayari amefanya kazi yake katika ripoti hiyo kuhusu ukiukaji wa mkataba na mikono yake “imefungwa zaidi ya hayo”.
Alisema kuwa jukumu ni la Bunge, kuchukua hatua zinazofaa baada ya mapendekezo yake.
“Jukumu la mwisho na jukumu la kuagiza kinachofaa kufanyika ni la Bunge,” alisema Bi Gathungu.