Habari

‘Nilikuwa mateka wa Al-Shabaab kwa miezi 19, niliyopitia hayasemezeki’

Na WAANDISHI WETU October 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Afisa wa Wilaya katika Kaunti ya Wajir, Bw Edward Yesse, amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu masaibu yake baada ya kutekwa nyara na wanamgambo wa Al-Shabaab, karibu miaka 13 iliyopita.

Mnamo Januari 2012, Bw Yesse alikuwa ameanza kazi yake mpya katika eneo la Burder, Wajir Kusini, na alitumwa katika eneo la Gerille, karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, kuendesha shughuli ya usajili wa vitambulisho kwa kushirikiana na Msajili wa Watu, Fredrick Wainaina, na maafisa wengine wa serikali.

Siku ya tatu baada ya kukamilisha shughuli hiyo, kundi la takriban wanamgambo 100 wa Al-Shabaab waliokuwa na silaha nzito walivamia kituo cha polisi walichokuwa, wakawashinda nguvu maafisa wa usalama na kuwateka nyara watatu wao – akiwemo Bw Yesse, Bw Wainaina na dereva wao.

Dereva aliachiliwa siku chache baadaye, lakini Yesse na Wainaina walivushwa mpaka hadi Somalia na kushikiliwa mateka kwa miezi 19 katika maeneo mbalimbali.

“Kuanzia wiki ya kwanza nilifungwa pingu, na siku ya sita tulipelekwa Mogadishu. Takriban asilimia 90 ya muda niliokuwa mateka ulikuwa wa mateso na hali mbaya ya kinyama,” alisema Bw Yesse.

Anasema walilazimika kutumia vyoo ndani ya seli walimokuwa, na mazingira yalikuwa machafu kupindukia. Walikuwa wakipewa chai nyepesi asubuhi na chajio jioni – mara mbili tu kwa siku.

Katika kipindi hicho, walihamishwa kutoka seli moja hadi nyingine zaidi ya mara 15, na kila mara walilazimishwa kurekodi video zenye ujumbe kwa serikali ya Kenya, kupitia Wizara ya Masuala ya Kigeni, wakieleza matakwa ya Al-Shabaab na kuomba kuokolewa.

“Watu waliokuja selini walijitambulisha kama Mujahideen. Walikuwa wakija mara kwa mara kutuhoji kuhusu masuala ya usalama na ujasusi,” alieleza.

Kwa sasa, Bw Yesse anaendelea na maisha yake kwa utulivu, lakini anasema kumbukumbu ya kipindi hicho bado inamsumbua.

Anaeleza kuwa alitekwa nyara kwa sababu ya maagizo ya kisiasa kuwalazimisha kuendelea na kazi licha ya ripoti za ujasusi kuonyesha hatari ilikuwepo eneo hilo.