Habari

‘Nilipoteza watoto wangu wote 6 kwa Mackenzie’

Na BRIAN OCHARO March 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BABA aliyepoteza watoto wake sita kwenye mauaji ya kutisha ya Shakahola, ameeleza masikitiko na jinsi hajapokea habari zozote kuhusu hatima yao hadi sasa.

Akitoa ushuhuda dhidi ya mhubiri Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake katika Mahakama ya Mombasa, Bw Mwiti alisema watoto hao walikuwa na mama yao, Bi Bahati Joan, katika msitu wa Shakahola tangu mwaka wa 2022. Mama huyo sasa ni mmoja wa washtakiwa.

“Sijapewa watoto wangu sita wala miili yao kwa ajili ya mazishi, licha ya kuwa nilitoa sampuli ya DNA kusaidia (serikali) kuwatambua. Tumesubiri kwa muda mrefu sana kwa sasa,” alimweleza Hakimu Mkuu Alex Ithuku.

Vifo vya Shakahola viligunduliwa mnamo Machi 2023, na zaidi ya miili 400 ikafukuliwa kutoka kwa makaburi ya kina kifupi.

Bw Mwiti, 47, alihuzunika kwamba sasa hana mtoto yeyote kwa sababu ya mafunzo ya Mackenzie, ambaye aliwapotosha mamia ya wafuasi wake, akiwemo mke wake.

Watoto hao walikuwa na umri wa kati ya miaka mitatu na 12.

“Nina miaka 47 sasa lakini sina mtoto yeyote, ilhali nilikuwa nao sita. Namlaumu Mackenzie kwa masaibu yangu,” alisema, akiongeza kuwa hatamhukumu Mackenzie, bali atamwachia Mungu.

Familia hiyo ilikuwa ikiishi Malindi, ambapo mkewe alikuwa akifanya biashara ya makaa na kushona nguo. Wote wawili walikuwa washirika wa Kanisa la Full Gospel.

Hata hivyo, mkewe alianza kufuatilia mahubiri ya Mackenzie kwenye runinga.

“Alisisitiza sana kutazama chaneli hiyo. Kisha akaniomba ruhusa ajiunge na kanisa la Furunzi, lakini nilikataa,” alisema.

Baadaye, mkewe aliacha kazi yake ya kushona nguo, na pia akaacha kupeleka watoto shule na hospitalini.

“Tulizozana, nikamwomba mamake aingilie kati kumshawishi aachane na mafundisho ya Mackenzie, lakini juhudi hizo hazikufua dafu,” alisema wakati akitoa ushahidi chini ya uongozi wa mawakili wa upande wa mashtaka, Jami Yamina, Victor Owiti, Alex Ndiema, Victor Simbi na Betty Rubia.

Alisema kuwa mkewe pia aliacha kupanga uzazi na hilo ndilo lilisababisha kuzaa watoto zaidi.

“Sikupanga kuwa na watoto wengi. Nilihitaji wawili tu. Watoto wa mwisho wanne walitokana na mafundisho ya Mackenzie.

Lakini niliwakubali kwa sababu walikuwa watoto wangu,” alisema, akiongeza kuwa hakuwahi kumwona mwanawe wa mwisho, aliyezaliwa msituni.

“Mke wangu alinipigia simu kunijulisha kuwa amejifungua mtoto wa kiume. Sikuwahi kumuona,” akaeleza wakati wa kuhojiwa na Bw Lawrence Obonyo, wakili wa Mackenzie.

Mnamo Agosti 20, 2022, Bw Mwiti aliondoka nyumbani mapema kwa shughuli zake, lakini aliporudi, alikuta nyumba yake ikiwa tupu.

Mkewe alikuwa ameondoka na watoto wao, na kuchukua chakula na Sh2,000.

“Sikuwa na wasiwasi mwanzoni kwa sababu alikuwa akitoweka na kurudi. Sikujua safari hii ingetofautiana,” alisema.

Mwanamke huyo alizima simu baada ya kuondoka. Kanisa la Furunzi lilikuwa limefungwa, jambo lililomfanya ashindwe mahali pa kumtafuta.

“Hadi leo, sijui watoto wangu walipo. Nimemwona mke wangu kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2022 leo,” alisema.