Niliwabwaga wazi Mbeere North, Wamuthende aambia Gachagua
MBUNGE mpya wa Mbeere Kaskazini, Leonard Njeru Wamuthende, amevunja kimya na kukiri kuwa kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo kilichokamilika majuzi hakikuwa mteremko.
Akizungumza na Taifa Dijitali, Bw Njeru alieleza kuwa alilazimika kupigana kisiasa, na kwa msaada wa Naibu Rais Kithure Kindiki na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku miongoni mwa maafisa wengine wa serikali kumshinda mpinzani wake wa karibu Newton Kariuki almaarufu Karish, aliyekuwa akiungwa mkono na upinzani.
“Yalikuwa mashindano makali, haikuwa safari rahisi kutokana na changamoto zilizojitokeza. Lakini kwa upinzani, ujumbe wangu ni kwamba nilishinda kihalali; tukutane 2027 kwa kinyang’anyiro kingine ambacho hakitakuwa rahisi kwao,” alisema Desemba 7, 2025 alipozuru wakazi wa Mbeere Kaskazini kwa mara ya kwanza tangu aapishwe.
Haya yanajiri huku wapiga kura wawili wakiwa tayari wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Embu wakitaka ushindi wake ubatilishwe, wakidai kulikuwa na makosa mengi kwenye uchaguzi wa Novemba 27.
Bw Njeru alisema anaunga mkono hatua hiyo kwani “ni haki yao ya kikatiba.”
Kulingana na Bw Wamuthende, upinzani ukiongozwa na kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua, ulivamia Mbeere Kaskazini kwa lengo la kumzuia asishinde na kuhakikisha chama cha UDA hakingepata kiti hicho.
“Upinzani uliwarai wakazi ili kupata huruma yao na kuninyima ushindi. Waliwaambia kuwa mwana wa Mlima Kenya alifurushwa serikalini na hivyo hawakufa kumpigia kura mgombea wa UDA,” alisema huku akiwashukuru wakazi kwa kumuunga mkono.
“Kulikuwa na mtu mwenye hasira aliyekuja hapa na kujaribu kuwashawishi wanikatae, lakini kwa bahati nzuri wakati ulipofika, wakazi walikuwa tayari wameamua,” alisema akimrejelea Bw Gachagua.
Bw Wamuthende alihusisha ushindi wake na kuuza ajenda yake ya maendeleo, kuungwa mkono na serikali, na umaarufu wa jina lake la ‘Wa Muthende.’
“Niliwaambia watu mipango yangu ya kuwaongezea umeme, maji, barabara na usawa katika ugawaji rasilmali, walisikiliza. Pia nilitumia jina la utani la babangu ‘Muthende’ ambalo linafahamika sana Mbeere. Upinzani haukuwa na ajenda; walitegemea matusi, propaganda na vurugu na walishindwa,” alisema.
Alikana madai kuwa alishinda kwa sababu serikali ilitumia Sh600 milioni kununua wapiga kura.
“Hakuna kiasi kama hicho kilitumika. Wakazi wa Mbeere Kaskazini walinipigia kura kwa sababu niliweza kueleza ajenda yangu. Pia nilifuata ushauri wa timu yangu ya kampeni kwa umakini, nikawashawishi wapiga kura,” alisema.
Miongoni mwa hoja zilizotajwa kuathiri kura ni koo, suala ambalo Bw Njeru alikiri lilimgonga kidogo. Hata hivyo aliukashifu mtindo huo kama “wa kizamani” na akaahidi kuwatumikia wakazi wote bila upendeleo.
“Nitahakikisha mgao wa basari unafanywa kwa haki na uwazi na kila shilingi ya NG-CDF inahesabiwa,” alisema.
Akaongeza: “Nataka kubadilisha maisha ya watu wa Mbeere Kaskazini kabla ya uchaguzi wa 2027. Tayari nimepata kilomita 68 za barabara ya lami na kwa kuwa niko serikalini nina imani milango itafunguliwa na watu wangu watanufaika.”
Bw Wamuthende alipata kura 15,802 dhidi ya 15,308 za mshindani wake wa karibu Newton Kariuki.