Habari

Nina mpango kabambe kwenu, Ruto aambia jamii za maeneo yaliyotengwa

Na NDUBI MOTURI December 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto Alhamisi, Desemba 18, 2025 alizindua mpango kabambe unaolenga makundi ya walio wachache na yaliyotengwa.

Mpango huo unajumuisha ufadhili wa elimu wa Sh500 milioni, bima ya afya kwa watu 200,000 walio hatarini, na mgao wa Sh200 milioni kila mwaka kuboresha shule na vyuo katika maeneo ambayo hayana huduma.

Rais alitangaza hayo katika Ikulu ya Nairobi wakati wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki za Walio Wachache na kuzinduliwa kwa Sera ya Kitaifa kuhusu Jamii za Wachache baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri.

“Mpango huo utatuwezesha kutekeleza Kifungu cha 56 cha Katiba, ambacho kinaitaka Serikali kulinda na kuendeleza haki za wachache na makundi yaliyotengwa,” Rais Ruto alisema.

Chini ya hatua hizo mpya, serikali itaanzisha mara moja Mpango wa Kitaifa wa Ufadhili wa Sh500 milioni kusaidia watoto kutoka “jamii za walio wachache na jamii zilizotengwa” kupata elimu ya sekondari na ya juu.

“Mpango huu utahakikisha kwamba umaskini sio kizuizi tena kwa talanta,” Rais Ruto alisema.

Kuhusu huduma ya afya, Serikali italipa ada za SHA kwa watu 200,000 walio katika mazingira hatari hasa kutoka kwa jamii ndogo na zilizotengwa, hatua ambayo Rais alisema “itahakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya na za bei nafuu” kwa watu ambao kihistoria wameachwa nje ya mfumo.

Wizara ya Elimu pia imeagizwa kutenga Sh200 milioni kila mwaka kama Hazina ya Miundombinu ya Elimu ili kujenga, kuboresha na kukarabati shule na vyuo vya ngazi ya kati katika maeneo yaliyotengwa.

“Hatua hizi sio maneno tu,” Rais Ruto alisema.

Sera mpya iliyozinduliwa inaweka mfumo mpana wa kufikia walio wachache, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Idara ya Jamii za Wachache na Jamii Zilizotengwa ndani ya Ofisi ya Rais na mipango ya Baraza la Kitaifa la Makabila madogo.