Yanayoweza yakafanyika Trump akidinda kumpongeza Biden au akatae kuondoka White House?
CHARLES WASONGA na MASHIRIKA
MASWALI yameibuka kuhusu kile kinachoweza kikafanyika ikiwa Rais Donald Trump atakatalia Ikulu ya White House ikizingatiwa kuwa hajaonyesha nia ya kukubali kushindwa na Joe Biden.
Mara baada ya mgombea huyo wa chama cha Democrat kuthibitishwa mshindi, Trump hakumtumia ujumbe wa pongezi kama ambavyo imekuwa ada kwa marais wa zamani walioshindwa.
Lakini swali ni je, nini kinaweza kikafanyika ikiwa Trump atakataa kuondoka Ikulu ya White House? Je, kuna Rais wa Amerika ambaye amewahi kudinda kuondoka Ikulu baada ya kushindwa?
Katika kujibu maswali haya tutarejelea tukio la mnamo Machi 4, 1801, nchini humo wakati ambapo Rais John Adams alikataa kumpokeza Thomas Jefferson afisi baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 1800.
Wakati huo, kanuni ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Amerika Januari 20 saa sita adhuhuri haikuwa imeanza kutumika.
Sawa na Trump John Adams ambaye ni Rais wa pili wa Amerika alikataa kutambua ushindi wa Jefferson na hivyo akakataa kumpokeza afisi.
Adams ambaye ndiye wa kwanza katika taifa hilo kushindwa kutetea kiti cha urais aliondoka jijini Washington, D.C., mapema asubuhi kwa kijigari kinachobururwa na farasi – stagecoach – kuepuka kabisa sherehe ya Jefferson kutawazwa rasmi kuiongoza Amerika.
Baada ya Jefferson kuapishwa katika hafla ambayo Adams alikataa kuhudhuria, wafanyakazi wa Ikulu ya White House walianza kutoa virago vya rais kutoka makazi hayo ya Rais. Shughuli hiyo iliendeshwa mchana peupe wananchi wakitazama.
Adams ndiye alikuwa Rais wa kwanza wa Amerika kuishi katika Ikulu hiyo baada ya ujenzi wake kukamilika.
Baada ya mali yake ya kibinafsi kuondolewa asasi zote za kuisalama zilikatiza mawasiliano kati yao na Adams. Wahudumu wote wa Ikulu walikoma kufuata maagizo yake na kuelekeza uaminifu wao kwa rais mpya, Jefferson.
Kwa kifupi Adams alivuliwa mamlaka kwa nguvu; akajipata bila afisi.
Kuanzia wakati huo, marais hujiandaa mapema kuondoka White House baada ya kuona dalili za kushindwa, ili kuzuia aibu kama iliyomfika Rais wa pili wa Amerika. Aibu hiyo ni kutoka kwa asasi huru za taifa hilo kama vile jeshi, vitengo vya ujasusi kama vile “The Secret Service, CIA, FBI na wahudumu wa Ikulu.
Asasi hizo zote zinahudumu chini ya sheria kwamba watatumikia mwanamume au mwanamke ambaye atapata idhini ya wananchi katika uchaguzi kuwa Rais wa Amerika.
Hii ndiyo maana Joe Biden alipopata zaidi ya kura za wajumbe 270 na kutambuliwa kuwa Rais Mteule wa 46 wa Amerika, mambo mengi yalianza kufanyika miongoni mwayo ni; kikosi cha Secret Service kimegawanya uaminifu baina ya rais wa sasa na rais mteule; CIA itaanza kuwasilisha habari za kijasusi kwa Biden sawa na inavyofanya kwa Trump, na muhimu zaidi ni kwamba maandalizi ya kumpokea Biden katika Ikulu ya White House mnamo Januari 20, 2021, yameanza.