Njama kuhakikisha Sakaja anapata useneta, Aladwa aponyoke na ugavana Nairobi
CHAMA cha ODM sasa kinalenga kiti cha ugavana wa Nairobi huku shinikizo za kichinichini sasa zikitaka Mbunge wa Makadara, George Aladwa, apokezwe tikiti ya kuwania ugavana mnamo 2027.
Haya yanajiri baada ya walioonekana hapo awali kutoroka ODM kuanza kuwa na miegemeo mingine ya kisiasa.
Mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi, aliyekuwa kifua mbele katika uwaniaji wa ugavana wa Nairobi 2022 lakini akaondolewa dakika za mwisho kupitia ushashawishi wa uongozi wa ODM, amehama siasa za jijini na analenga kuwania ugavana Kaunti ya Bungoma.
Hata huko huenda Bw Wanyonyi asipate wakati rahisi kwa sababu kiti hicho kinamezewa mate na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, wawili hao wakitarajiwa kung’ang’ania kiti cha Ford Kenya.
Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, naye anaonekana kuasi siasa za ODM na kuegemea mrengo wa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka huku akilenga kura za jamii ya Wakamba na Ukanda wa Mlima Kenya.
Kuondoka kwa wawili hao kumeacha ODM ikijikuna kichwa huku chama hicho hapo awali kikionekana kuegemea mrengo wa Gavana Johnson Sakaja.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa ODM sasa wanaona Bw Sakaja atakuwa mzigo kwa chama hicho kutokana na utendakazi duni na sasa wanaunga mkono Bw Aladwa apokezwe tikiti ya ugavana Nairobi 2027.
Kinara wa ODM Raila Odinga ameonekana kuingilia kati na kumrai Bw Aladwa asalie katika siasa za jijini badala ya kuwania kiti cha ugavana wa Vihiga jinsi ambavyo mbunge huyo alivyolenga hapo awali.
“Naunga mkono Bw Aladwa kwa ugavana Nairobi kwa sababu amesimama sana na chama hapa jijini. Pia anatoka jamii ya Mulembe ambayo ina wapiga kura wengi sana Nairobi na tayari amechangamkiwa na wengi,” akasema Afisa wa Nyanjani wa ODM kutoka Kangemi, Christopher Ongara.
Mwenyekiti wa ODM kitengo cha walemavu Kennedy Omollo naye alisema kuwa wakati umefika ambapo juhudi za Bw Aladwa kusimama na ODM Nairobi zithaminiwe na wana hakika akipokezwa tikiti, atawabwaga wapinzani mapema asubuhi.
“Bw Aladwa amekuwa Meya jijini na tuliona jinsi ambavyo kulikuwa na mpangilio. Jiji lilikuwa safi, wachuuzi hawakuwa wakihangaishwa na amelelewa hapa jijini kwa hivyo, anafahamu jinsi ya kuliongoza,” akasema Bw Omollo.
Viongozi wengi nyanjani wamewataka Rais William Ruto na Bw Odinga watumie ushirikiano wao kuhakikisha kuwa Bw Aladwa anaendea ugavana huku Bw Sakaja akipokezwa tikiti ya kuwania useneta.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Aladwa alikiri kwamba Bw Odinga amemshawishi asiende kuwania ugavana Vihiga na abakie Nairobi kwa ‘kiti kikubwa’ zaidi kuliko ubunge.
“Nimekuwa kwa hiki chama kwa kipindi kirefu na ninaelewa sana siasa za Nairobi. Baba (Raila) aliniamnbia nisiende Vihiga na nimetii, nitabaki hapa katika siasa za Nairobi,” akasema Bw Aladwa.