Njama ya kuzima Orengo 2027 yasukwa
MGAWANYIKO katika chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga unaendelea kupanuka huku ripoti zikieleza kuhusu mpango wa siri wa Serikali kumzima Gavana wa Siaya, James Orengo, katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 kutokana na msimamo wake dhidi ya serikali Jumuishi.
Inadaiwa kuwa mpango huu unahusisha wapangaji mikakati wa ngazi za juu ndani ya Serikali Jumuishi, ukilenga kumzima kisiasa wakili huyo kwa sababu ya kuikosoa vikali.
Gavana Orengo, mshirika wa karibu wa Bw Odinga na sauti ya muda mrefu ya siasa za upinzani, amekuwa wazi katika kukosoa utawala wa Rais William Ruto, akimlaumu kwa ufisadi, usimamizi mbaya wa uchumi, na ukiukaji wa haki za binadamu.
Huku baadhi ya viongozi wa ODM, akiwemo Waziri wa Kawi, Opiyo Wandayi, Waziri wa Hazina ya Taifa, John Mbadi, Waziri wa Madini, Hassan Joho, na Waziri wa Ushirika, Wycliffe Oparanya, wakijiunga na serikali ya Rais Ruto chini ya serikali Jumuishi iliyoundwa kufuatia maandamano ya Gen Z mwaka jana, Gavana Orengo ameendelea kuwa mkosoaji bila kukoma.
Vyanzo vya kisiasa katika Nyanza sasa vinasema kuwa serikali inakusudia ‘kupunguza nguvu za Orengo’ kabla ya uchaguzi ujao.
Awali, wanachama wa kundi la wataalamu kutoka jamii ya Waluo walitaka kumng’atua gavana, hatua ambayo hawakutekeleza, huku madiwani wa Siaya wakikataa kuhudhuria mkutano wa hivi karibuni katika Ikulu ya Nairobi.
Kiongozi wa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG), David Ochieng’, ambaye pia ni Mbunge wa Ugenya na mshirika wa zamani aliyegeuka kuwa mkosoaji wa Orengo, ni miongoni mwa wapinzani wanaoweza kufadhiliwa kumzima.
Bw Ochieng’ alitangaza hadharani kuwa yuko tayari kugombea ugavana wa Siaya ikiwa Orengo atashindwa kutekeleza jukumu lake.
‘Raila amesema kwamba hata kama kura zake ziliibiwa, alilazimika kushirikiana na Rais Ruto kumsaidia kuimarisha serikali na kwa upande wake, rais amekubali kusaidia eneo letu katika masuala ya maendeleo, lakini gavana Orengo anaendelea kumdharau,’ alisema Bw Ochieng’ wiki iliyopita.
Aliongeza: ‘Jukumu la gavana ni kuimarisha maendeleo na kufanyia kazi watu wake na ikiwa Orengo hawezi kufanya hivyo basi niko tayari kumkabili debeni ili kusaidia watu wetu.’
Katika wiki chache zilizopita, Gavana Orengo amekumbana na mashambulizi kutoka kwa wafuasi wa serikali jumuishi kaunti ya Siaya, wakiwemo Waziri Opiyo Wandayi, Seneta wa Siaya, Oburu Oginga, na Mbunge wa Alego Usonga, Sam Atandi.
‘Gavana wa Siaya lazima aache uanaharakati na aelekeze nguvu zake kuhudumia watu waliomchagua. Wabunge, na kwa kiasi fulani Seneti, ndio wanapaswa kushiriki katika kile ambacho gavana anajaribu kufanya,’ alisema Bw Wandayi.
Dkt Oginga alidai: ‘Ikiwa (Orengo) anajihisi kutofurahishwa na ODM kufanya kazi na serikali, basi anaweza kujiuzulu kutoka chamani kabisa.’
Inaripotiwa kuwa Bw Wandayi amekuwa akifanya mikutano Nairobi, na amewakaribisha viongozi kadhaa kutoka kaunti ya Siaya, wakiwemo Dkt Oginga, Bw Ochieng’, aliyekuwa Waziri Raphael Tuju, aliyekuwa Mbunge wa Rarieda, Nicholas Gumbo, na Naibu Gavana wa Siaya, William Oduol. Mikutano ya wakosoaji wa gavana inaonekana kama juhudi za kumdhibiti kisiasa.
Mwenyekiti wa ODM wa Kaunti ya Siaya, Oloo Okanda, alisema wanajua kuhusu mpango wa serikali kumfadhili mgombea dhidi ya Bw Orengo kutokana na msimamo wake kuhusu serikali jumuishi.
‘Tuna taarifa za kuaminika kuhusu hili kwamba kumekuwa na mikutano ya kujaribu kupata mgombea anayeweza kushindana na Orengo katika 2027 huku kiongozi wa chama, Raila Odinga mwenyewe, akitangaza kuwa ODM inabaki kuwa upinzani,’ Bw Okanda aliambia Taifa Leo.
Bw Odinga ametetea Bw Orengo, Gavana wa Kisumu, Prof. Anyang’ Nyong’o, na Katibu Mkuu wa ODM kutokana na kauli zao za kukosoa serikali, akisema pia anaunga maoni yao.
Wiki iliyopita, alitofautiana na Dkt Oginga, kaka yake mkubwa, kuhusu msimamo wa ODM, akisisitiza kuwa yuko katika upinzani na si sehemu ya serikali.
Bw Sifuna aliambia Taifa Leo kuwa hakuwa na habari kuhusu mpango wa serikali kufadhili mgombea dhidi ya Bw Orengo na akasisitiza kuwa ODM haina uhusiano na serikali na inabaki kuwa upinzani.
‘Ninaendelea kusema kuwa hakuna serikali inayoitwa jumuishi. Tuna Serikali ya Kenya Kwanza na wote wanaohudumu ndani yake wanamfanyia kazi Ruto. Mkataba wetu na UDA ni mfumo wa ushirikiano tu ulioundwa kwa kuzingatia maslahi ya pamoja,” alisema Bw Sifuna kwa Nation.
Wachambuzi wa siasa wanahisi hali katika kaunti ya Siaya ni mfano wa mvutano mpana zaidi ndani ya ODM, huku chama kikikabiliana na mabadiliko ya ndani na mabadiliko ya kimkakati ya kisiasa ya Bw Odinga baada ya 2022.