Njiraini amezea mate kiti cha Swazuri
Na CHARLES WASONGA
ALIYEKUWA Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), John Njiraini na aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini, Esther Murugi ni miongoni mwa watu 11 watakaohojiwa kwa wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC).
Wengine walioorodheshwa kwa nafasi hiyo ambayo zamani ilishikiliwa na Profesa Muhammad Swazuri, ni mtaalamu wa masuala ya ardhi, Mwenda Makathimo, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Wanawake Naomi Wagereka na wakili Gershom Otachi.
Wengine ni; Mbw Robert Kipkosgei Kilimo, Humprey Njuguna, Hussein Farah, Patrick Adolwa, Paul Wambua na Galgalo Ali.
Mwenyekiti wa Jopo la uteuzi wa makamishna wa NLC Priscilla Nyokabi alisema kuwa shughuli ya kuwahoji watu hao itaanza Jumatatu juma lijalo.
“Kamati ya uteuzi inathibitisha kuwa watu walioorodhesha watafanyiwa mahojiano katika afisi za Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), orofa ya nne katika Commission House jijini Nairobi katika tarehe na saa iliyotajwa kwenye tangazo hili. Watakaohojiwa wanatakiwa kufika mahala hapo angalau muda wa nusu saa kabla ya saa iliyowekwa,” akasema Nyokabi kwenye tangazo lilichapishwa magazetini Jumanne.
Stakabadhi ambazo watu hao wanahitajika kubeba ni pamoja na nakala za kitambulisho cha kitaifa, vyeti vya masomo na taaluma. Pia wanahitaji kubeba vyeti vya kuonyesha kuwa hawadaiwi na Bodi ya Kutoa Mikopo kwa Elimu ya Juu (Helb), KRA, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Afisi ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Nafasi za makamishna
Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri wa Leba, Bw Kazungu Kambi, aliyekuwa Katibu wa Wizara, Khadija Kassachoon na aliyekuwa Mbunge wa Mugirango Kusini, Omingo Maraga ni miongoni mwa watu 50 walioorodheshwa kuhojiwa kwa nafasi saba za makamishna ya NLC.
Watakaoteuliwa watajaza nafasi iliyoachwa wazi na makamishna wanane ambao muda wao wa kuhudumu ulikamilika mnamo Aprili mwaka huu.
Wao ni aliyekuwa naibu mwenyekiti wa NLC Bi Abigael Mbagaya na makamishna; Bw Clement Lenachuru, Bi Emma Njogu, Bw Sila Muriithi, Bw Abdikadir Adan Khalif, Dkt Rose Musyoka, Dkt Samuel Tororei na Dkt Tom Konyimbili Mboya.
PSC ilisema kuwa ilipokea maombi kutoka kwa jumla ya watu 117 kwa wadhifa wa mwenyekiti huku wengine 940 wakiomba nafasi za kuwa makamishna.
Profesa Swazuri, Bi Mbagaya, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Tom Chavangi na maafisa wengine wa NLC wanakabiliwa na kesi kuhusu sakata mbalimbali za ufisadi.
Mojawapo ni ulipaji wa takriban Sh230 milioni kinyume cha sheria, kama fidia kwa wale ambao ardhi yao ilitwaliwa kupisha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).