Habari

NLC: Tiya Galgalo atemwa na wabunge

September 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wamekataa kuidhinisha uteuzi wa Tiya Galgalo kuwa kamishna wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) baada ya kubainika kuwa hakuwa ametimiza masharti ya ulipaji ushuru.

Kamati ya Bunge kuhusu Ardhi ilisema kwenye ripoti yake iliyowasilishwa bungeni Jumatano kwamba cheti cha ushuru ambacho Bi Galgalo aliwasilisha mbele yake wakati alikuwa akihojiwa kwa wadhifa huo wiki jana kilikuwa ni feki.

“Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) imepinga uhalali wa cheti hicho. Hii ina maana kuwa Bi Galgalo bado kutimiza masharti ya ulipaji ushuru na hivyo hawezi kuruhusiwa kushikilia wadhifa wa umma,” kamati hiyo ikasema katika ripoti hiyo iliyotiwa saini na mwenyekiti wake Rachael Nyamai.

Kamati hiyo ambayo ilikwenda Mombasa wikendi iliyopita kuandika ripoti hiyo ilisema Mwakilishi huyo wa Wawake wa zamani wa Isiolo hakufuata utaratibu ufaafu kupata cheti hicho.

Kamishna Mkuu wa KRA James Mburu wiki jana aliambia kamati hiyo kwamba Bi Galgalo hakulipa ushuru kwa mapato yake katika miaka ya 2017 na 2018.

Bw Mburu alisema mamlaka hiyo imeanzisha uchunguzi kubaini jinsi mwanasiasa huyo alipata cheti cha ushuru kisicho halali, kisha awasilishe ripoti kwa wabunge.

Hata hivyo, Bi Galgalo alikana madai ya kushiriki udanganyifu ili kupata stakabadhi hiyo, akisema cheti hicho kilitumwa kwa anwani yake ya baruapepe baada ya kujaza mahitaji mitandaoni.

“Tunachunguza wafanyakazi wetu kubaini ni nani alimsaidia kupata cheti feki,” Bw Mburu akaambia kamati hiyo katika ukumbi wa County Hall, Nairobi.

Hata hivyo, kamati hiyo iliidhinisha majina wa watu wengine nane waliopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kujaza nafasi za mwenyekiti na makamishna wa tume hiyo.

Wao ni; Gershom Otachi (Mwenyekiti) pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Esther Murugi, Bi Getrude Nguku, Bw Reginalda Okumu, aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Egerton Profesa James Tuitoek na aliyekuwa mbunge wa Kaloleni na Waziri wa Leba Samuel Kazungu Kambi. Wengine ni; Bw Hubbie Hussein Al-Haji, Bw Alister Murimi Mutugi.