Habari

Nyanya wa miaka 75 ashtakiwa kwa ulaghai wa shamba la Sh200 M

Na RICHARD MUNGUTI November 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MJANE mwenye umri wa miaka 75 alishtakiwa Novemba 10, 2025 kwa kula njama kumlaghai mwanasiasa wa jijini Nairobi Agnes Kagure Kariuki shamba lenye thamani ya Sh200 milioni.

Ruth Wambui Kimani ambaye alikuwa kitembea kwa msaada wa mkongojo alimweleza hakimu mkazi mahakama ya Milimani Rose Ndombi kuwa “nimeshtakiwa bure. Shamba ninalodaiwa kulaghai ni mali ya mume wangu Francis Kimani Mungai almaarufu Kimani Mungai aliyeaga. Mimi ndiye msimamizi na mdhibiti wa mali yake.” Nyanya huyo aliyekuwa ameandamana na mjukuu wake alitetewa katika kesi hiyo na wakili Peter Mirie.

Bw Mirie aliyeomba korti imwachilie nyanya huyo kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu alifichua kwamba kuna kesi iliyoshtakiwa 2018 na bado haijasikizwa na Mahakama kuu.

Katika kesi hiyo Bi Kimani pamoja Joseph Mwangi Njeri wamewashtaki Agnes Kagure Kariuki, Francis Kimani Mungai na Kimemia Enterprises Company Limited.

Bw Mirie alieleza mahakama kwamba mshtakiwa (Ruth Wambui Kimani) anaomba mahakama kuu ifitulie mbali hati ya umiliki wa shamba hilo nambari LR.No.209/4843/10 (IR No15372) iliyopewa Agnes Kagure Kariuki na wizara ya ardhi.

“Bi Kimani mwenye umri wa miaka 75 amefikishwa kortini kwa sababu ya kutetea mali yake,” Bw Mirie alieleza mahakama.

Wakili huyo alisema mshtakiwa ndiye mrithi wa mali ya mumewe na kamwe hapasi kushtakiwa kwa uhalifu ambao hajafanya.

Katika kesi iliyoko mahakama kuu Jaji Charles Mbogo alifahamishwa na Agnes Kagure kwamba aliuziwa shamba hilo la ukubwa wa hektari 0.3252 kwa bei ya Sh10milioni.

Mahakama ilielezwa kesi hiyo ya Mahakama kuu itaanza kusikizwa Novemba 19 na 20 2025.

Hakimu aliombwa amwachilie mshtakiwa kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu ikitiliwa maanani ni kikongwe na anaugua.

“Mshtakiwa alitiwa nguvuni Ijumaa na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na kuagizwa afike kortini,”alisema Mirie.

Mahakama iliambiwa ilibidi maafisa wa polisi wamnunulie dawa mshtakiwa baada ya kuugua.

Walimwachilia kutoka kizuizini na kumtaka afike kortini Jumatatu Novemba 10,2025.

Hakimu aliombwa amwonee huruma nyanya huyo na kumwacha kwa dhamana afya yake isidorore akiwa gerezani.

Katika uamuzi wake Bi Ndombi alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu.

Aliamuru kesi hiyo itajwe Desemba 8,2025 kutengewa siku ya kusikizwa.

Upande wa mashtaka uliagizwa umkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi ndipo atayarishe ushahidi wake.