Habari

Nyota waeleza siri ya kung’aa katika mtihani wa KJSEA

Na WAANDISHI WETU December 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA kundi la kwanza la wanafunzi waliofanya Mtihani wa Gredi 9 (KJSEA) mafanikio hayakuja kwa bahati.

Mafanikio hayo yalitokana na uvumilivu, muda mrefu wa masomo, fikra za haraka na msaada thabiti kutoka kwa wazazi na walimu waliokuwa pamoja nao katika safari hii.

Kama kundi la kwanza la mfumo mpya wa elimu, walikosa mfano wa kuiga au watahiniwa waliowatangulia wa kuuliza, bali walitegemea azma yao katika mazingira ambayo hawakuwa na uzoefu.

Effie Rhodil Achieng kutoka Shule ya Hekima, Kisumu, ambaye alipata alama 69, aeleza kuwa mafanikio yake yalitokana na imani yake kwa Mungu, walimu na wazazi waliomsaidia kila mara alipoona mambo yanakuwa magumu.

“Kama darasa la kwanza, ilikuwa changamoto kwani hatukuwa na mtu wa kuiga. Tulijiandaa kwa KJSEA na KPSEA( wa darasa la sita) ambayo ni ngumu, lakini kwa ujasiri na motisha kutoka kwa kila mtu aliye karibu nasi, tuliweza kufanikiwa,” alisema Rhodil.

Kwa Candy Praise, ambaye alifanya mtihani huo katika shule hiyo hiyo na kupata alama sawa, walikuwa wamejiandaa vizuri na walitarajia matokeo mazuri.

“Tulitarajia matokeo mazuri na ndiyo tulipata kupitia nidhamu na msaada wa walimu pamoja na motisha binafsi,” alisema Praise ambaye anatarajia kujiunga na Shule ya State House Girls au Moi Kabarak.

Hata hivyo, mwenzake Nevine Imani alikiri kuwa tathmini hiyo ilikuwa changamoto kubwa.

“Nilihisi wasiwasi kuhusu mitihani na matokeo, lakini kupitia nidhamu, uvumilivu, kazi ngumu na uthabiti, nilifanikiwa,” alisema Imani aliyepata alama 69.

John Gospel kutoka Shule ya Msingi ya Arya, Kisumu, alipata alama 70, huku Terrence Allen wa Shule ya Msingi ya Xaverian akipata 65.Akipokea matokeo yake, Gospel mwenye umri wa miaka 15 alikiri mafanikio yake yalitokana na msaada wa familia na walimu wake.

“Kama si kwa wazazi wangu na walimu, singeweza kupata matokeo haya chanya,” alisema.

Terrence Allen, ambaye alieleza kuridhika kwa alama 65, alikiri juhudi za pamoja zilizochangia mafanikio yake.

“Nimefurahi sana. Nilipata msaada mkubwa kutoka kwa wazazi, walimu na marafiki. Kufika hapa hakukuwa rahisi,” alisema.

Allen alihusisha mafanikio yake na ndugu yake, Valarie Gloria, ambaye alimsaidia wakati wa kipindi cha mtihani.

“Nataka kuwa rubani na ninaamini nitakuwa rubani bora katika miaka ijayo,” alisema.

Kaunti ya Migori ilirekodi alama ya juu zaidi katika eneo hilo, ambapo Telsa William kutoka Rongo Success Academy alipata alama 71.

Mwenzake, Carina Rozenberg Ojwang, alipata alama 67.

William alihusisha mafanikio yake na kuamini Mungu na ushauri wa walimu waliojitolea kwa dhati.

Victor Makes Bala na Gabriel Otieno wa Siaya Central Comprehensive School wanasema kwamba uvumilivu, kazi ngumu na uthabiti vinaweza kuzaa matokeo baada ya kupata alama 70 kila mmoja, jambo lililopatia shule yao sifa kubwa.