ODM kifua mbele Msambweni – Utafiti
Na MOHAMED AHMED
MWANIAJI ubunge katika eneo la Mswambweni kwa tiketi ya chama cha ODM, Bw Omar Boga, angeibuka mshindi ikiwa uchaguzi huo mdogo ungefanyika leo, umeonyesha utafiti mpya.
Utafiti huo, ambao matokeo yametolewa Alhamisi na shirika la Trends and Insights for Africa Research (TIFA), ulionyesha kuwa Bw Boga angepata asilimia 54 ya kura, huku asilimia 29 wakimpigia Bw Feisal Bader, anayegombea kama mwaniaji wa kujitegemea.
Bw Ali Hassan Mwakulonda wa chama cha Peoples Economic Democracy (PED) angeibuka wa tatu kwa kuzoa asilimia tisa ya kura. Bw Mwarere Wamwachai angeibuka wa nne kwa kupata asilimia mbili ya kura.
Hata hivyo, utafiti ulionyesha asilimia mbili ya wapigakura hawajui mwaniaji watakayempigia kura. Idadi kama hiyo ilikataa kueleza mwaniaji watakayempigia kura.
Utafiti huo ulifanyika kati ya Novemba 29 na Desemba 1 kutoka kwa wakazi 320.
Utafiti huo pia ulionyesha asilimia 48 ya wenyeji wanaunga mkono ODM huku asilimia 24 wakiunga mkono Chama cha Jubilee (JP).
Asilimia tatu wanaunga mkono chama cha Wiper, huku kiwango kama hicho wakiunga mkono PED. Asilimia nne ilieleza kuunga mkono vyama vingine vya kisiasa.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 42 ya wale watakaopiga kura walisema watarejelea shughuli zao za kawaida huku asilimia 43 wakisema matokeo hayatawaathiri hata kidogo.
Asilimia saba ilisema kutakuwa na wizi wa kura, asilimia tatu ikaeleza kuhofia kuambukizwa virusi vya corona, nayo asilimia nne ya wenyeji ikaeleza kuhofia ghasia kuzuka.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa Bw Boga ndiye anayefahamika zaidi na wapigakura kwa kiwango cha asilimia 43, akifuatwa na Bw Bader kwa asilimia 36.
Asilimia 42 ilitaja manifesto ya Bw Boga kama sababu kuu ya kumfahamu kwa kina, huku asilimia 48 ya wale wanaomfahamu Bw Bader ikitaja utendakazi wake.
Bw Bader ndiye aliyesimamia Hazina ya Eneobunge (CDF) wakati marehemu Bw Suleiman Dori alipohudumu kama mbunge wa eneo hilo.
Wakati huo huo, asilimia 34 ya wenyeji walisema wanampendelea Bw Boga kutokana na utendakazi wake. Bw Boga alihudumu kama diwani wa wadi ya Bongwe/ Gombato kati ya 2013 na 2017.
Hata hivyo, ripoti ilieleza kuwa huenda matokeo ya utafiti huo yakatofautiana na matokeo halisi ya uchaguzi huo, kwani huenda baadhi ya wapigakura waliosajiliwa humo lakini wanaishi nje ya eneo hilo wakashiriki. Uchaguzi umepangiwa kufanyika Desemba 15.