Habari

Oguna awaomba raia, wanahabari kuwa na subira shughuli ya uopoaji ikiendelea

October 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

RABSHA zimetokea katika kivuko cha feri Likoni baada ya umati uliofika eneo hilo kufuatilia shughuli ya uopoaji wa gari na miili ya mwanamke na mwanawe kukabiliana na vyombo vya dola.

Wengine waliingia ndani ya feri na kususia hatua yoyote ya kutiwa nguvuni.

Maafisa wa jeshi ambao wamekuwa wamemwagwa katika eneo hilo kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa walilazimika kutumia nguvu kudhibiti umati huo.

Operesheni hiyo ambayo iko kwa juma la pili imekuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu mkubwa kutoka kwa Wakenya na raia wa nchi jirani.

Msemaji wa serikali kanali mstaafu Cyrus Oguna amesema amewaomba Wakenya kuwa na subira ili kuwapa waopoaji muda na mazingira muafaka kukamilisha operesheni ya kuopoa miili ya Bi Miriam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu.

Shughuli ya uopoaji inaendelezwa na shirika la utoaji huduma za feri (KFS) mamlaka ya bandari (KPA), kikosi maalum cha ulinzi baharini (KCGS) na taasisi ya utafiti wa baharini.

“Hii si shughuli rahisi; inahitaji tajiriba na ushirikiano wa hali ya juu kufaulu,” amesema Oguna.

Aliyekuwa waziri mkuu Rails Odinga alipofika katika kivuko cha Likoni Feri kuipa moyo familia ya Bi Kighenda alisema ajali hiyo inaonyesha utepetevu katika shirika la huduma za feri.

“Hii inaonesha mtu mmoja alizembea katika kazi yake. Hata hivyo, huu si wakati wa kunyoosheana kidole cha lawama bali wakati wa kuitakia utulivu familia,” alisema Raila.

Mkasa huo uliotokea Septemba 29, 2019, ulifanya Wakenya wengi kuinyooshea serikali kidole cha lawama maafisa wa kikosi cha wanamaji na shirika la huduma za feri kwa ‘utepetevu’.

Bi Mariam Kighenda na mwanawe walizama katika kivuko cha feri Likoni baada ya gari lao aina ya Toyota ISIS lenye nambari za usajili KCB 289C kuteleza kutoka ndani ya feri MV Harambee na kutumbukia ndani ya maji.