Habari

Orengo: Mkifukuza Sifuna ODM inaisha

Na DAN OGETA January 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

VIONGOZI wa ODM wanaompinga Dkt Oburu Oginga wameendelea kushinikiza chama hicho kiandae Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) ili kuwateua maafisa wapya.

Wakiongea walipohudhuria ibada ya kanisa mtaa wa Kawangware, Nairobi, Jumapili, walisema jaribio lolote la kumfukuza Katibu Mkuu Edwin Sifuna halitafaulu.

“Nataka kuwaambia kuwa iwapo mtu atathubutu kumfukuza au kumwondoa Sifuna kama katibu mkuu, hiyo itakuwa mwisho wa ODM,” akasema Gavana wa Siaya James Orengo.

Gavana huyo pia alisisitiza kuwa familia ya Raila Odinga pamoja na watoto wake lazima waheshimiwe. Bw Orengo alisema matamshi ya kweli ya marehemu Raila yapo katika aliyoyasema akiwa hai na maandishi yaliyomo katika ajenda 10 ODM ilitia saini na UDA.

Alisema Bw Sifuna alikuwa kati ya waliotia saini hoja hizo 10 kwa hivyo anafahamu anachokisema iwapo anaibua malalamishi.

Gavana huyo alisema muafaka kati ya ODM na UDA ulikuwa wa kushusha gharama ya maisha na si kuunda muungano wa kisiasa.

“Kwa hivyo, msidanganywe kwa sababu Raila hakusema chochote kuhusu kuungana kisiasa na yeyote. Alisema haki za Wakenya ndizo zinakuja kwanza kisha baadaye ndipo angeamua kuhusu mwelekeo wa kisiasa,” akasema Bw Orengo.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alimuunga mkono Bw Orengo akisema hakukuwa na muafaka kati ya Raila na Rais Ruto kuhusu 2027.

“Ni vyama hivyo ndivyo vilimjia na kama wandani wake tutasimama na kile alichosema kinachofahamika wazi,” akasema Bw Owino.

Bw Osotsi naye alisema ODM ni chama cha Wakenya na hawatakubali kimezwe kutimiza maslahi ya viongozi wachache.