Orengo motoni kwa kukosoa Raila
UHUSIANO baridi wa kisiasa kati ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na Gavana wa Siaya James Orengo unazidi kuchacha, ukiibua kumbukumbu za mvutano wao uliotokana na siasa za mageuzi miaka ya 1990.
Huku Bw Odinga akiendelea kuimarisha ushirikiano wake na Rais William Ruto kupitia mkataba kati ya ODM na UDA, Gavana Orengo anaonekana kupinga wazi hatua hiyo, akikosoa muafaka huo na kuonya dhidi ya ushirikiano usio na msingi katika siasa.
Katika mazishi ya mlinzi wa karibu wa Bw Odinga, George Oduor, yaliyofanyika Siaya, Orengo aliwashangaza wengi kwa kutoa matamshi yaliyoonekana kumlenga moja kwa moja Raila na washirika wake wapya serikalini.
“Sitakuwa kwenye kwaya ya sifa. Tulipigania kidemokrasia katika Katiba inayowapa watu haki ya kusema ukweli. Kutumia mfumo wa sheria kwa njia ya kulipiza kisasi lazima kukome,” alisema Orengo huku akiongeza kuwa maendeleo ya kaunti ya Siaya ni haki wala si zawadi kutoka kwa serikali.
Ingawa viongozi wengine waliokuwa kwenye hafla hiyo, akiwemo kaka wa Raila, Dkt Oburu Oginga, Mbunge Junet Mohamed, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, waliunga mkono ushirikiano wa ODM na serikali ya Kenya Kwanza, Orengo alichukua msimamo tofauti, akisisitiza kuwa si kila mtu anaweza kuwa serikalini, bali ni bora kupigania haki.
Matamshi yake yamezua hisia kali kutoka kwa viongozi wa Nyanza, hasa kutoka kwa kundi la wataalamu wa eneo hilo, Ramogi Professionals Caucus, ambao walimtuhumu Orengo kwa kuchochea uhasama wa kisiasa na kuvuruga mshikamano wa jamii ya Waluo.
“Kauli ya Orengo haiwakilishi Mluo yeyote. Tunamuunga mkono Raila katika mkataba wake wa kisiasa na Rais Ruto kwa sababu umerejesha utulivu na kuleta maendeleo,” alisema mwenyekiti wao Joshua Nyamori.
Baadhi ya viongozi wametishia kuanzisha mchakato wa kumbandua Orengo kutoka wadhifa wake wa ugavana kwa tuhuma za “utovu wa nidhamu na usaliti wa kisiasa”.
Oscar Omondi, aliyewahi kugombea useneta wa Siaya, alisema “ikiwa Gavana Orengo hataomba msamaha, tutaanzisha mchakato wa kumbandua kwa mujibu wa Katiba. Tumepoteza mengi kwa sababu ya upinzani, sasa tunahitaji maendeleo.”
Kauli hii imeungwa mkono na viongozi wengine wa ODM kama vile Mbunge wa Alego Usonga Sam Atandi na Bi Rachel Omollo wa Ramogi Caucus, waliomshauri Orengo aache siasa za misimamo mikali na badala yake asimamie maendeleo ya kaunti yake.
Licha ya shinikizo hizo, Orengo hajatoa kauli yoyote hadharani kuhusu mzozo huo, hatua ambayo baadhi wanaichukulia kama ishara ya kutorudi nyuma. Wachambuzi wanasema msimamo wake unakumbusha mwaka 2021 alipopinga hadharani mpango wa BBI, uliosukwa na Raila na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Uhasama kati ya Raila na Orengo una historia ndefu tangu kifo cha Jaramogi Oginga Odinga, ambapo Orengo alimpinga Raila kama kiongozi wa Ford Kenya, na kusababisha mgawanyiko wa kisiasa katika jamii ya Waluo. Tangu wakati huo, wawili hao wamekuwa na uhusiano wa kuaminiana japo kwa tahadhari.
Sasa, tofauti zao kuhusu ushirikiano mpya kati ya ODM na serikali ya Ruto zinaonekana kufufua uadui huo wa zamani, wakati huu kwa muktadha mpya wa kisiasa.