Habari

Orengo yu mzima kiafya, Raila aondolea hofu wakazi wa Siaya

Na KASSIM ADINASI July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KINARA wa ODM Raila Odinga amewatuliza wakazi wa Kaunti ya Siaya kwa kuwaambia kwamba Gavana James Orengo yuko imara kiafya na atarejelea majukumu yake hivi karibuni.

Gavana Orengo hajaonekana hadharani kwa muda naye Naibu Gavana Oduol Denge hajakuwa akijihusisha na masuala ya kaunti baada ya kukosana na uongozi wa sasa.

“Nimesikia watu wakiuliza gavana yuko wapi. Nataka kuwahakikishia kuwa yuko salama na atarejea hivi karibuni,” akasema Bw Odinga.

Waziri huyo mkuu wa zamani alikuwa akiongea wakati wa mazishi kwenye Shule ya Msingi ya Bar Atheng’ eneobunge la Ugunja wikendi.

“Orengo ni kama ndovu ambaye kukosekana kwake kunafanya watu wanongónezane, Hata hivyo, msiwe na wasiwasi, atarudi,” akaongeza Bw Odinga.

Kukosekana kwa gavana huyo na kutengwa kwa Bw Oduol kumewaingiza wasiwasi wakazi ambao baadhi wamekuwa wakiuliza nani anasimamia kaunti.

Mkazi Julius Oluoch tayari ameandikia barua Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC), Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini, Seneti na Chama cha ODM kuhusu kile alichosema ni ‘pengo la uongozi’

Bw Oluoch alisema kuwa kukosekana kwa Bw Orengo kumesababisha majukumu ya kaunti yakwame ikiwemo kuidhinishwa kwa Bajeti ya 2025/26.

“Kwa mwezi moja sasa, gavana hajaonekana  na shughuli za kaunti zimesimama ikiwemo kupitishwa kwa bajeti ya 2025/26,” akasema.

Mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu serikalini alithibitishia Taifa Leo mnamo Julai 17, kuwa Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti alimwaandikia Waziri wa Fedha wa kaunti kuhusu kucheleweshwa kwa budget.