Orengo yuko wapi? Maswali kuhusu anayesimamia kaunti gavana akitoweka mwezi mzima
WAKAZI wa Siaya wamezua maswali kuhusu aliko Gavana wao James Orengo baada ya kiongozi huyo kukosa kuonekana hadharani kwa karibu mwezi mmoja sasa.
Wasiwasi umeibuka kuhusu jinsi ambavyo shughuli za kaunti zinaendeshwa wakazi wakitaka uwajibikaji kutoka kwa viongozi ambao wamekuwa usukani wakati Bw Orengo hayuko.
Ikizingatiwa kwamba hakuwa akionana uso kwa macho na Naibu Gavana Oduol Denge, wengi sasa wanashangaa nani anasimamia kaunti.
Kikatiba Bw Oduol anastahili kusimamia kaunti kama gavana hayuko lakini uhusiano wao uliharibika kabisa naibu huyo wa gavana akionekana kutomakinikia shughuli za kaunti.
“Mbona Oduol asiruhusiwe asimamie kaunti kama Orengo hayuko?” akauliza.
Bw Oduol hapo awali alisema kuwa alinyimwa nafasi ya kurejea afisini na alikuwa amejaribu mara kadhaa kuridhiana na gavana ili arejee ofisini lakini akashindwa.
“Afisi yangu haitambuliwi kabisa na utawala wa sasa,” alisema Bw Oduol huku akifichua kuwa hata gari lake ramsi halijazwi mafuta na kaunti tena.
Mmoja wa wafanyakazi wa kaunti ambaye hakutaka anunukuliwe alisema Bw Oduol hajawahi kualikwa kwenye mikutano ya baraza la mawaziri.
“Wakati ambapo gavana hayuko mawaziri wamekuwa wakihusika na kuendesha shughuli za kila siku za kaunti,” akasema.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Siaya George Okode naye alikanusha madai kuwa amekuwa akisimamia kaunti wakati ambapo Gavana Orengo hayuko.
“Gavana amekuwa akiwakilishwa kwenye shughuli mbalimbali za kaunti na maafisa tofauti wakiwemo madiwani na mwenyekiti wa Bodi ya Uajiri. Kuwakilishwa ni jambo la kawaida,” akasema Bw Okode.
“Ni kweli gavana haonekani moja kwa moja lakini huwa anawasiliana na mawaziri wake na viongozi wengine kuhusu yanayoendelea. Teknolojia inamruhusu kuongoza kutoka mahala popote,” akaongeza.