OUKO: Ofisi ya mkaguzi wa hesabu za serikali inahitaji uadilifu
Na CHARLES WASONGA
EDWARD Ouko aliyekamilisha kipindi chake akiwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameelezea ni kwa nini ofisi hiyo ni mojawapo ya ofisi huru za kikatiba zenye wajibu mkubwa serikalini.
Kwa hivyo, anashauri kuwa uteuzi wa atakayejaza nafasi yake unafaa kuendeshwa kwa makini ili kupatikane mtu ambaye atafanya kazi kitalaamu pasina kuyumbishwa na mirengo mbalimbali ya kisiasa.
“Hii ni kazi ngumu inayohitaji mtaalamu mkakamavu kwa sababu inahusu ukaguzi wa utendakazi wa serikali kuu iliyoko mamlakani. Ni wajibu ambao utakuweka katika hali ya kukwaruzana na wanasiasa kila wakati kwa sababu oafisi hii ni kiungo muhimu katika mchakato mpana wa vita dhidi ya ufisadi,” akasema Bw Ouko.
Hii ndio maana kwa kipindi cha miaka minane ambayo amekuwa oafisini tangu ateuliwe mnamo Agosti 27, 2011, Ouko amekuwa akikwaruzana na watumishi wa umma na wanasiasa kiasi kwamba mnamo 2017 kulikuwa na jaribio la kumwondoa ofisini kupitia Bunge la Kitaifa.
Baadhi ya maafisa wakuu katika serikali ya Jubilee, na wanasiasa watetezi wa serikali, walikuwa na wasiwasi kwamba ufichuzi wa kila mara wa wizi wa pesa za umma, kupitia ripoti za ofisi ya Bw Ouko, ungezima mustakabali wao kisiasa kwa kudhoofisha umaarufu wao miongoni mwa wapigakura.
Ni watu kama hao ambao inadaiwa walichochea njama ya kumng’oa Ouko ofisini kupitia ombi lililowasilishwa na wakili Emmanuel Mwagambo Mwagona.
Mlalamishi huyo alimhusisha Bw Ouko na sakata ya utoaji zabuni ya Sh100 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya matumizi katika oafisi yake pamoja na uajiri wa wafanyakazi kwa mapendeleo.
Hata hivyo, njama hiyo ilizimwa na Jaji George Odunga (wakati huo akihudumu katika mahakama ya kuu) ambaye alisema kuwa bunge lilikiuka Katiba kwa kumnyima Bw Ouko haki ya kumhoji mlalamishi jinsi inavyohitajika chini ya kipengee cha 47 cha Katiba.
Yamkini, hakuna ofisi imeufanya umma kuangazia vita dhidi ya ufisadi na wizi wa pesa za umma kuliko Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali tangu enzi za utawala wa Kanu.
Na imefanya hivyo kwa uendelevU kupitia ripoti za kila mwaka ambazo huangazia visa kadha vya watumishi wa umma kutumia vibaya mamlaka yao kwa kuiba fedha.
Ripoti za Bw Ouko zilitumiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuendesha chunguzi ambazo zilisababisha Ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuwafungulia mashtaka washukiwa kadhaa wa ufisadi.
Kutokana utendakazi wake, Bw Ouko hakuwa na marafiki wengi serikalini.
Baadhi ya maafisa wa serikali walidai alikuwa kibaraka wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye aliyelenga kuiharibia sifa ili kumfaidi (Bw Odinga) kisiasa.
Hata hivyo, mwaka 2018 Bw Ouko alipata tuzo kutokana na hali kwamba afisi yake ilizingatia utaalamu na uwazi katika utekelezaji wa Mbinu Mpya za Ukaguzi.
Alipokea Tuza kwa jina ‘The Regularity (Financial) Audit Award of Recognition’, ambayo inasawiriwa kuwa kielelezo cha utendakazi wake tangu alipoteuliwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwa wadhifa huo mnamo Agosti 27, 2011.
Hii ndio maana Bunge la Seneti linakubaliana na kauli ya Bw Ouko kuwa mchakato wa kuteua yule atakayechukua nafasi hiyo unapaswa kuendeshwa kwa uangalifu ili kuhakikisha kuwa utendakazi wa ofisi hiyo, hasa vita dhidi ya ufisadi haviyumbishwi.
“Atakayeingia katika ofisi hii sharti awe mtu mwenye sifa sawa na Bw Ouko. Mtu mweledi kazini na ambaye atazingatia utaalamu katika kazi yake,” akasema Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (CIPAC) Moses Kajwang.
Bw Kajawang ambaye ni Seneta wa Homa Bay akaongeza: “Hatutaki kuona utendakazi wa afisa huyo mpya ukiingiliwa jinsi Ouko alivyofanyiwa. Kazi ya afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali inapasa kuheshimiwa katika sababu hii ni ofisi ya kikatiba na nguzo kuu utendakazi wa serikali.”
Vitisho
Mwanasiasa huyo pia alitoa mfano wa hapo awali ambapo Rais Uhuru Kenyatta alimkaripia Bw Ouko katika Ikulu ya Nairobi kuhusu uchunguzi aliokuwa akiendeshwa kuhusu sakata ya Eurobond, akisema vitisho kama hivyo havifai kuelekezewa ofisi hiyo.
Kulingana Katiba, naibu wa Bw Ouko hawezi kutwaa mamlaka ya ofisi hiyo hadi pale utendakazi wake (Bw Ouko) utakapofanyiwa ukaguzi.
Hii ndio maana Ouko amekuwa akiishinikiza Bunge kuteua Mkaguzi huru atakayeifanyia ukaguzi ofisi yake kwa mujibu wa hitaji la kipengee cha 226 cha Katiba ya sasa.
Ukaguzi huo utahusisha utendakazi wa afisi hiyo kuanzia mwaka wa kifedha wa 2014/ 2015 kuendelea mbele.
Hivi majuzi bunge la kitaifa, kupitia Kamati ya Uhasibu (PAC) ilikodi huduma za kampuni ya uhasibu wa PKF Kenya kufanya ukaguzi katika afisi hiyo kabla ya Bw Ouko kuondoa rasmi.
Ingawa umma ulichangamkia utendakazi wa Bw Ouko, anaondoka bila furaha kutoka na hali kwamba mapendekezo mengi kwenye ripoti ambazo amekuwa akitoa kila mara huwa hayatekelezwi.
Ripoti hizo ambazo huwasilishwa bungeni (katika kamati ya PAC) hufichua visa kadha vya wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Inasikitisha kuwa siasa zimekuwa zikiingizwa katika mapendekezo hayo na kupelekea kupuuzwa kwao. Hii ndio maana wengi wa maafisa waliohusika katika wizi wa pesa za umma wangali huru mpaka sasa,” anasema Bw Ouko.
Anapendekeza mabadiliko katika Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM Act) na Sheria kuhusu Ukaguzi wa Asasi za Umma (Public Audit Act) ili Ofisi wa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali iwe na mamlaka ya kuwalazimisha wezi wa pesa za umma wazirejeshe, kama inavyofanyika katika mataifa ya Ghana na Afrika Kusini.
Bw Ouko ni mwanachama na mshirika wa Taasisi ya Wahasibu wa Uingereza na Wales ambako anawakilisha Afrika.
Vilevile, yeye ni mwanachama wa Taasisi ya Uhasibu Nchini Kenya (ICPA).
Alipata Shahada ya Digrii Taaluma ya Masuala ya Usimamizi wa Kifedha Uhasibu.
Kabla ya kuteuliwa kama Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Kenya Bw Ouko alihudumu kwa miaka 24 kama Mkaguzi wa Hesabu katika Benki ya Maendeleo Afrika, ambako alisimamia kitengo cha kupambana na ufisadi.
Vilevile amewahi kufanya kazi nchini Uingereza na kampuni ya Deloitte nchini Kenya.