Habari

Oyamo aomba aondolewe lawama ya kumuuwa Sharon

Na RICHARD MUNGUTI May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MICHAEL Oyamo, mshukiwa wa pili katika mauaji ya kinyama ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno miaka minane iliyopita alikamilisha tetezi zake huku akiomba mahakama kuu imwondolee lawama.

Sharon aliuawa pamoja na mtoto wake aliyekuwa kuzaliwa kwa kudungwa kwenye kitovu na fito ya chuma kikatokea upande wa mgongo.

Walikufa papo hapo.

Kabla ya kumtoa Sharon uhai, majambazi waliotekeleza uhaifu huo walimbaka.

Maiti yake ilikutwa ndani ya msitu Homa-Bay baada ya kuripotiwa amepotea.

Sharon alikuwa ametekwa nyara pamoja na mwanahabari anayetambuliwa kwa jina XYZ kwa sababu ya usalama wake.

Mwanahabari huyo na Sharon waliabiri teksi nje ya hoteli ya Gracia iliyoko Homa Bay kupelekwa kukutana na gavana wa zamani wa Migori Okoth Obado.

XYZ aliruka kutoka kwa gari lililokuwa linawapeleka kwa Gavana Obado na kuponya nafsi yake.

XYZ ndiye alifichua kisa cha kutekwa nyara kwa Sharon na kupiga ripoti kituo cha Polisi.

XYZ anayelindwa na Serikali alikuwa ameombwa na Sharon achapishe katika Gazeti kuhusu mimba yake na uhusiano wake na Gavana.

Sharon alifikia uamuzi huo baada ya Obado kukwepa kuwasiliana naye ilhali alikuwa amebeba mimba ya mtoto wake.

Akijitetea mbele ya Jaji Cecilia Githua , Oyamo aliwasilisha ushahidi kutoka kampuni ya mawasiliano ya Safari-com kuthibitisha hakuwa mahala Sharon alipouliwa.

Msaidizi huyo wa Obado, aliwaaga Sharon na XYZ katika hoteli ya Gracia kisha akaabiri Boda Boda kumpeleka nyumbani kwake Migori mnamo Septemba 3,2018, usiku ule Sharon aliuawa.

Keshoye Septemba 4,2018 Oyamo aliambia mahakama alipokea simu nyingi kwamba amehusishwa na mauaji ya Sharon.

Alikuwa ameanza safari ya Nairobi alipokuwa anaungana na Obado kusafiri hadi Rwanda kwa kongamano la Magavana.

“Nilirudi Migori kutoka Kisii. Nilirudisha marupurupu ya pesa tulizokuwa tumepewa na kaunti ya Migori. Niliamuru dereva arudishe gari kwa afisi za kaunti kisha nikajisalamisha kwa Polisi kituo cha Uriri,” Oyamo alimweleza Jaji Githua.

Alikamatwa na kuhojiwa na makachero kutoka Nairobi na Migori.

Hatimaye alisafirishwa hadi Nairobi na kushtakiwa kwa mauaji ya Sharon na mwanawe.

Obado, Oyamo na aliyekuwa mfanyakazi wa kaunti ya Migori Casper Obiero wamekana shtaka la kumuua Sharon mnamo Septemba 3 na 4,2018.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma DPP Renson Ingonga  aliomba kesi hiyo iahirishwe had Juni 11,2025 kumwezesha kukagua ushahidi mpya aliowasilisha Oyamo kutoka kwa kampuni ya Safari-com ndipo amhoji zaidi kuhusu mauaji hayo ya Sharon.