Passaris atishia kumchukulia Sonko hatua kali za kisheria
Na MWANGI MUIRURI
MASAIBU ya Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kuhusu tabia na mienendo yake ya kijamii na kisiasa sasa yamechukua mwelekeo mpya baada ya Mwakilishi Mbunge Mwanamke eneo hilo, Esther Muthoni Passaris kusisitiza kumshtaki.
Bi Passaris akiongea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta alipotua nchini kutoka ziara ya kikazi nchini Canada alisema kuwa “Sonko amezidi.”
Shida kati yao wawili ziliibuka katika maadhimisho ya makala ya 56 ya Madaraka Dei ambapo Bi Passaris alirukia Sonko katika hotuba yake akimwangazia kama “Gavana aliye na pesa nyingi na ambazo huzigawa bila mpangilio na ambapo taswira ni kwamba hela hizo ni haziwezi kuelezeka zilikotoka.”
Aliteta kuwa Gavana Sonko huwa haungi mkono miradi ya umoja wa viongozi wa Nairobi bali yeye hupenda tu kufanya mambo yake kivyake.
Aidha, aliteta kuwa Gavana Sonko huwa na mazoea ya kukwepa kuafikika na viongozi wengine kiasi cha kukataa kupokea simu akimpigia.
Ni kwa msingi huo ndipo Sonko alizindua misururu ya kisasi, akianza kwa kumsuta Passaris kuwa mwanamke asiye na maadili mema kuhusu mapenzi, akateta kuwa hawezi akapokea simu kila mara amempigia kana kwamba yeye ni mumewe, na cha mno, akaingia katika runinga ya Citizen kusambaza dhana hizo za shaka kuhusu ulainifu wa kimaadili wa mwanasiasa huyu wa ODM jijini Nairobi.
Sasa, Bi Passaris anasema kuwa hatapambana na Sonko katika safu hiyo ya kujibizana maneno pasipo mpangilio wa kufuata mkondo wa kisheria.
“Kuna wandani wangu walionitaka nimjibu Sonko mara moja aliponigeuza kuwa vibonde kwa msingi huo wake wa utundu wa ulimi lakini
sitafuata mkondo huo wa utukutu. Nitawasilisha lalama zangu rasmi kwa idara ya uchunguzi wa jinai nchini (DCI) na pia katika tume ya maadili
na kupambana na ufisadi (EACC),” akasema.
Pia, alisema kuwa atawasilisha malalamishi katika afisi ya Tume ya Uwiano wa Kitaifa (NCIC).
“Nitatumia kila fursa ya kisheria ilio wazi kuhakikisha kuwa huu ni wakati wa mwisho tunamsikia akitumia ulimi mchafu kwa mwingine yeyote,” akasema.
Alihuzunika kuwa maneno ya Sonko “yalinikera na kuniaibisha hasa ikizingatiwa kuwa mimi ni mama kwa watoto wawili wazima na pia mke wa mtu.”
Ingawa Sonko hudai hadharani kuwa “nina pesa, uwezo na nia ya kupambana mahakamani kuhusu kila aina ya kesi, ni wazi kuwa katika mahakama ya umma kuhusu tabia zake na mienendo katika masuala mengi, ashahukumiwa kuwa anahitaji kudhibitiwa.
Tabia yake ya kurekodi kila aina ya maongezi yake na wanaompigia simu imetajwa na wengi kama “ushenzi” huku viongozi wengi wakimkashifu si haba kwa kutodhibiti ulimi wake anapofanya maongezi hadharani.