Habari

Patrick Ole Ntutu afurushwa na wabunge

October 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Jumanne, waziri mwingine msaidizi amekabiliwa na wakati mgumu katika majengo ya bunge pale wabunge walikataa kumtambua kama mwakilishi rasmi wa waziri anayesimamia wizara anayohudumia.

Bw Patrick Ole Ntutu ambaye ni Waziri Msaidizi katika Wizara ya Usalama wa Ndani inayoongozwa na Dkt Fred Matiang’i amefurushwa kutoka kikao cha Kamati ya Bunge kuhusu Usalama wanachama waliposema cheo chake hakitambuliwi katika Katiba ya sasa.

Bw Ole Ntutu alikuwa ametumwa na Waziri Matiang’i kujibu maswali kutoka kwa wabunge kwa niaba yake ikizingatiwa kwamba alikuwa amebanwa na shughuli nyinginezo za afisi yake.

“Kipengee cha 153 (3) kinasema wazi kwamba Waziri ndiye anapaswa kufika mbele ya kamati za bunge kujibu masuala yaliyoulizwa na wabunge wala sio watu wengine ambao wanaitwa CASs (mawaziri wasaidizi),” amesema Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi.

Kauli yake imeungwa mkono na wenzake, Aduma Owuor (Nyakach), Mohammed Kolosh (Wajir Magharibi), David Sankok (Mbunge Maalum) miongoni mwa wengine.

Hapo ndipo Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo John Waluke alipomwamuru Bw Ole Ntutu aende akamwambie Dkt Matiang’i yeye ndiye anahitajika kujibu maswali.

“Rudi afisini umwambie Dkt Matiang’i aliyekutuma hapa kwamba yeye ndiye tunamhitaji hapa kwa sababu cheo unachoshikilia hakitambuliwi na Katiba,” akasema Bw Waluke.

Wiki jana wabunge wanachama wa Kamati ya Afya pia walikataa waziri msaidizi wa Afya Dkt Rashid Amana ambaye alimwakilisha Waziri Sicily Kariuki.

Walichukua hatua hiyo baada ya Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa kudai kuwa uteuzi wa maafisa hao (mawaziri wasaidizi) ulifanywa kinyume cha katiba.

Spika Justin Muturi anatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu suala hilo wiki hii.

Muturi atatoa uamuzi kuhusu iwapo ni halali kisheria kwa mawaziri wasaidizi (CASs) kufika mbele ya kamati za bunge kujibu maswali kwa niaba ya mawaziri.

Hii ni baada ya wabunge wengi wiki jana kusema kuwa hawatawatambua mawaziri hao wasaidizi kama wawakilishi rasmi wa mawaziri kwa misingi kwamba “nyadhifa zao hazitambuliwi kwenye Katiba”

Wiki jana Bw Barasa alikataa kabisa majibu yaliyotolewa na Dkt Amana akisisitiza kuwa hamtambui kama afisa ambaye ana uwezo wa kumwakilisha Waziri wa Afya.

“Sitakubali majibu yaliyosomwa na Dkt Amana kwa niaba ya Waziri Kariuki kwa sababu cheo anachokishikilia cha Waziri Msaidizi hakitambuliwi katika Katiba ya sasa,” akasema Bw Barasa kabla ya kuwasilisha ombi maalum kwa Spika Muturi akitaka ufafanuzi rasmi kuhusu iwapo maafisa hao wana mamlaka kisheria kuwasilisha misimamo rasmi ya Wizara.

Wabunge wengi waliochangia hoja kuhusu suala hilo mnamo Jumatano alasiri wiki jana walikubaliana na kauli ya Bw Barasa kwamba bunge halifai kutambua mawaziri hao wasaidizi (CASs).

Ikiwa Bw Muturi atataoa uamuzi unaokubaliana na msimamo wa wabunge, mawaziri watakoma kuwatuma CASs hao kujibu maswali kwa niaba yao katika kamati za bunge.

Mvutano

Hatua hiyo huenda ikaibua mvutano mpya katika ya bunge na serikali kuu ikizingatiwa kuwa mawaziri wengi hukosa kufika mbele ya kamati za bunge kwa sababu ya kuzidiwa na majukumu mengine.

Kukosa kwao kufika kumewakera wabunge kiasi cha baadhi yao kutisha kudhamini hoja ya kutokuwa na imani na mawaziri hao.

Katika uamuzi wake Bw Muturi atategemea kipengee cha 153 (3) cha Katiba kinachosema kuwa ni wajibu wa Mawaziri kufika mbele ya Kamati za Bunge la Kitaifa au Seneti wanapoitwa kujibu maswali yanayohusiana na masuala ya wizara zao.

Lakini katika siku za hivi karibuni, mawaziri wengi wamekuwa wakipitisha wajibu huo kwa mawaziri wasaidizi.

Hatua hiyo imewakasirisha wabunge ambao wanadai kuwa Waziri aliye na wajibu wa kujibu maswali hayo kama mtu binafsi na hafai kuupitisha kwa afisa mwingine.

“Huu ni wajibu ambao Waziri hafai kumpa mtu mwingine. Hitaji la Katiba ni kwamba Waziri afike mbele ya kamati ya bunge,” akasema Mbunge wa Ugenya David Ochieng’.

Kauli yake iliungwa mkono na kiongozi wa wengi Aden Duale aliyesema: “Nadhani Katiba imesema wazi kuwa huu ni wajibu wa Waziri. Tunamtaka Spika kutoa mwelekeo kwa sababu tulikubaliana kuwa ikiwa Waziri anahisi kuwa hawezi kufika mbele ya kamati, yu huru kuomba kufika wakati mwingine.”

Duale ni Mbunge wa Garissa Mjini.

Hata hivyo, alitetea hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuunda nyadhifa hizo akisema washikilizi wazo wanaweza kusaidia katika masuala ya usimamizi.

Lakini kiongozi wa wachache alikosoa hatua ya Rais ya kubuni nyadhifa hizo akisema hazitambuliwi katika katiba ya sasa.

Hata hivyo, kipengee cha 132 cha Katiba kinampa Rais mamlaka ya kubuni nyadhifa serikalini lakini baada ya kushauriana na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC).