Peleka matapishi huko nje, Oburu afokea Orengo kwa kukosoa Serikali Jumuishi
SENETA wa Siaya Oburu Oginga amemshutumu vikali Gavana wake James Orengo kwa kuendelea kuikosoa serikali jumuishi akimtaka kugura ODM ikiwa hajaridhishwa na ushirikiano kati ya chama hicho na chama cha UDA.
Dkt Oginga amemkumbusha Bw Orengo na wanasiasa wengine wanaopinga ushirikiano huo, akisema ulitokana na uamuzi wa pamoja wa ODM wala sio mtu mmoja.
“Wale ambao wanapinga serikali jumuishi akiwemo gavana wangu wanatutapikia. Waondoke wakatapike huko nje. Sisi katika ODM tunataka kupumua hewa safi katika ushirikiano wetu na chama cha UDA,” akasema Dkt Oginga.
Dkt Oginga, ambaye ni kaka mkubwa wa kiongozi wa ODM Raila Odinga, alimtaka gavana Orengo kuwahudumia wakazi wa Siaya waliomchagua badala ya kudai kila mara kwamba anapigania haki zake.
“Wajibu wake kama gavana ni kuwafanyia kazi wakazi wa siasa, sio kudai kila mara kwamba anapigania haki zao. Tayari tunapigania haki za watu wetu tukiwa bungeni huku Rais akitekeleza wajibu wake wa kuongoza. Wewe kama gavana wajibu wako ni kuwahudumia wananchi sio kushiriki katika siasa,” Dkt Oburu akaeleza.
Seneta huyo alisema hayo Jumapili mjini Migori alipohudhuria ibada maalum ya madhehebu mbalimbali iliyohudhuriwa na Rais William Ruto.
Dkt Oburu alisema hayo siku moja baada ya Bw Orengo kuapa kuendelea kukashifu kile alichokitaja kama tishio kwa utawala wa kidemokrasia na utawala wa sheria nchini Kenya.
Akiongea Jumamosi katika eneo bunge la Ugenya, Kaunti ya Siaya, Bw Orengo alisisitiza kuwa hatakubali kunyamazishwa na vitisho anavyoelekezewa kutoka na msimamo wake.
“Sharti tuwe na uongozi unaozingatia utawala wa sheria na unaoheshimu Katiba na ukweli. Siwezi nikachelea wajibu wangu kwa Wakenya na nchi yangu kwa kukosa kusema ukweli,” akaeleza.
Bw Orengo alikuwa akiongea katika Zahanati za Urenga na Bar Ndege alipozindua mradi wa upanuzi wa miundomsingi katika vituo hivyo vya afya.
Na akiongea Aprili 12, wakati wa ibada ya kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa mlinzi wa Bw Odinga, marehemu George Oduor, Bw Orengo aliapa kutojiunga na wanasiasa wa ODM wanaoisifu serikali kikasuku.
“Siwezi kuwa kiongozi wa kuisifu serikali bila kuhoji maovu yake. Tulipania Katiba hii ili Wakenya waweze kuwa na uhuru wa kusema. Nawahimiza Wakenya wawaambie viongozi wao ukweli. Nchi hii itaangamia tena ikiwa semi ninazosikia zitaendelea,” Orengo akaeleza.
“Maendeleo yanayoletwa katika kaunti ya Siaya ni haki ya wakazi wala sio zawadi,” Bw Orengo akaeleza.