Pendekezo vijana wasio na kazi wapewe Sh48,000 na serikali
Na PETER MBURU
WABUNGE wawili wanapendekezea bunge kubadili sheria, ili vijana ambao hawajaajiriwa wawe wakipewa kiwango fulani cha pesa na serikali, kama mbinu ya kuwakinga kutokana na hali ngumu ya maisha.
Wabunge Caleb Amisi (Saboti) na Didmus Barasa (Kimilili) wanalitaka bunge kubadili sheria kuhusu Uajiri na Huduma za Kijamii, ili vijana ambao hawana kazi wawe wakipewa Sh48,000 kila mwaka na serikali, sawa na Sh3,000 kila mwezi.
Viongozi hao aidha wamependekeza kuwa wanafunzi wanaofuzu kwa Diploma ama Shahada ya kwanza wawe wakilipwa Sh25,000 wanapochukuliwa kufanya kazi za kimafunzo (internship).
Endapo bunge litapitisha pendekezo hilo, ambalo mwanzilishi wake ni Bw Amisi, kila kijana asiye na kazi atakuwa akipewa Sh12,000 na serikali kila baada ya miezi minne.
“Watu wasio na kazi Kenya hawalipwi marupurupu ya kukosa kazi na misaada yoyote ya kimaisha kama jinsi ilivyo katika mataifa mengine. Vijana wengi hawawezani na maisha ya mijini ambapo ndipo nafasi za ajira zinapatikana,” Bw Amisi akasema.
Mbunge huyo alijutia kuwa vijana wengi wanakosa kupewa misaada na ufadhili ambao utawawezesha kupata ajira ili wajitegemee wenyewe.
Kulingana na ripoti ya punde zaidi kutoka kwa shirika la kimataifa la UNDP, vijana wapatao milioni 2.6 hawana kazi nchini, licha ya kuwa wengi wao wana ujuzi wa kufanya kazi mbali mbali na wanazitafuta.
Hii ni kumaanisha kuwa serikali itatumia jumla ya Sh93.6 bilioni kuwalipa vijana hao mwaka wa kwanza, kiwango ambacho kitapanda hadi zaidi ya Sh100 bilioni mwaka wa pili.
Bw Barasa naye anataka wanafunzi wa Diploma na Shahada wanaofuzu wawe wakipewa kazi za kimafunzo na mashirika ya serikali na ya kibinafsi, na kulipwa Sh25,000 kila mwezi.
“Mswada huu unataka wanafunzi hao walipwe pesa chache zaidi ambazo zinaruhusiwa kwao,” Bw Barasa akasema.
Kulingana na sheria ya sasa kuhusu utoaji wa misaada ya kijamii kwa watu, watu wenye uhitaji wa misaada hiyo pekee ndio wanaruhusiwa.
Watu waliotajwa ni mayatima, watoto wasio na uwezo, wazee maskini, wasio na kazi, walemavu, wajane na wengine ambao waziri anaweza kuruhusu.
Wabunge hao walikuwa mbele ya Kamati ya Bajeti bungeni Jumanne ambapo waliwasilisha miswada yao, na kutetea jinsi itafadhiliwa.