Pengo katika ofisi ya msimamizi wa bajeti laathiri serikali za kaunti
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI za kaunti zimeshindwa kuwalipa wafanyakazi wao mishahara baada ya kukabiliwa na changamoto ya kuitisha pesa kupitia ofisi ya Msimamizi wa Bajeti (CoB).
Hii ni baada ya kukamilika kwa muda wa kuhudumu wa Stephen Masha ambaye alishikilia wadhifa huo kama kaimu kwa siku 90.
Bw Masha ndiye alikuwa akitoa idhini kwa serikali za kaunti kutoa fedha kutoka akaunti zao katika Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwa matumizi mbalimbali ikiwemo ulipaji wa mishahara.
Mnamo Agosti 28, 2019, Rais Uhuru Kenyatta alimteua Bw Masha kuwa kaimu CoB baada ya muda wa kuhudumu wa Agnes Odhiambo kukamilika.
Alihudumu katika wadhifa huo kwa siku 90 hadi Novemba 25, 2019, na baada ya hapo ofisi hiyo imesalia wazi.
Hii ndiyo maana kulingana na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Wycliffe Oparanya, sasa serikali za kaunti haziwezi kutoa fedha za matumizi kwa sababu hamna afisa wa kuzipatia idhini ya kufanya hivyo.
“Kutokana na hali hii, serikali za kaunti zimeshindwa kutoa malipo mbalimbali yakiwemo mishahara ya Novemba, fedha zinazofaa kulipa asasi za serikali, pesa za kununulia huduma na mahitaji ya kila siku na malimbikizo ya madeni,” akasema Bw Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kaunti ya Kakamega.
“Kwa hivyo, kaunti zote 47 hazijapokea mgao wao Sh31.6 bilioni wa mwezi wa Novemba, pesa ambazo zilistahili kutolewa mnamo Novemba 15, 2019,” akaongeza.
Kwa hivyo, Bw Oparanya ameitaka Serikali ya Kitaifa kuharakisha mchakato wa kujaza nafasi ya mshikilizi mpya wa ofisi ya CoB ili aweze kuidhinisha kutolewa kwa fedha za kaunti kufanikisha mipango ya utoaji huduma.
“Pia serikali inafaa kuwasilisha fedha zote ambazo ilistahili kuwa zimetolewa kufikia Novemba 15 ili kaunti ziweze kulipa madeni yao,” aliongeza.
Wiki jana, Rais Uhuru Kenyatta alimpendekeza Bi Margaret Nyakango, ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Kifedha katika Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), kuchukua nafasi ya Bi Odhiambo.