PIC yaamuru ukaguzi wa benki ya NBK huku ikipinga kuuzwa kwake
BUNGE la kitaifa limeitaka Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko kuifanyia ukaguzi benki ya National (NBK) kwa muda wa wiki mbili.
Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) ilisema Alhamisi kuwa benki hiyo iliuzwa kwa bei ya chini kwa benki ya Kenya Commercial (KCB) na hivyo thamani yake kamili inafaa kukadiriwa na afisi ya Bw Ouko.
Usimamizi wa NBK umepinga shughuli hiyo ya ukaguzi na afisi ya mkaguzi mkuu ukisema kuwa benki hiyo ni ya kibinafsi.
Benki ya KCB imetangaza kuwa inanunua asilimia 100 ya hisa za NBK kwa kubadilisha hisa moja ya KCB na kila hisa 10 za NBK.
Mpango huo ambao umeidhinishwa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) unatarajiwa kufufua shughuli za benki hiyo (NBK) ambayo imekuwa ikipata hasara.
Mfumo huo wa kubadilishwa kwa hisa za benki hiyo ya kitaifa unaweka thamani yake kuwa Sh6.6 bilioni.
Kamati ya PIC, inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir, imekosoa mpango huo wa uuzaji wa NBK kwa benki ya KCB.
PIC imeelezea hofu kwamba masilahi ya wafanyakazi wa sasa, wale waliostaafu na walipa ushuru hayatalindwa chini ya mpango huo.
“Tumekagua hali ya hisa katika NBK, mali yake, madeni yake na mpango mzima wa uuzwaji wake na kubaini kuwa haina manufaa yoyote na una madhara mengi kuliko faida,” akasema Bw Nassir
Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) inamiliki asilimia 48.1 ya hisa za benki hiyo (NBK) ambayo imeorodheshwa katika soko la hisa la Kenya.
Kwa upande mwingine, Hazina ya Kitaifa inamiliki asilimia 22.5 ya hisa huku hisa zilizosalia zikimilikiwa na umma.
PIC imeiamuru NBK kuwasilisha vitabu vyake vyote vya akaunti kwa Afisi ya Bw Ouko kwa ukaguzi na kumtaka mkaguzi huyo mkuu kuwasilisha ripoti yake kuhusu hali ya kifedha ya benki hiyo baada ya kipindi cha siku 14.